Kimataifa

Mkosoaji wa Rais Kagame azimwa kuwania urais

June 9th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

KIGALI, RWANDA

MKOSOAJI Mkuu wa Rais wa Rwanda Paul Kagame, Diane Rwigara, amezuiwa kushiriki katika kinyang’anyiro cha urais nchini humo mnamo Julai 15, 2024.

Ni Bw Kagame na wanasiasa wengine wawili – Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na mgombeaji huru Philippe Mpayimana – walioidhinishwa na tume ya uchaguzi kuwania kiti hicho.

Bi Rwigara, ambaye pia alizimwa kuwania katika uchaguzi wa 2017 alitumia mtandao wa kijamii wa X kulalamika na kumlaumu Kagame kwa kuchochea kuzuiwa kwake kuwania urais.

“Mbona unakataa kuniruhusu kuwania? Hii ni mara ya pili ambapo ameninyima haki yangu ya kuendesha kampeni na kushiriki uchaguzi wa urais,” akasema.

Bi Rwigara, mwenye umri wa miaka 42 na ambaye ni kiongozi wa Chama cha People Salvation Movement (PSM), awali aliwaambia wanahabari kwamba alikuwa na matumaini makubwa kwamba mwaka huu angewania wadhifa huo wa urais.

“Nawakilisha idadi kubwa ya raia wa Rwanda ambao wanaishi kwa woga na hawaruhusiwi kufurahia uhuru katika nchi yao,” akasema.

“Rwanda inachukuliwa kama nchi ambayo uchumi wake unakua. Lakini mashinani, hali ni tofauti. Watu wanakosa mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, maji na nyumba,” Bi Rwigara akasema.

Tume ya Uchaguzi ilipotoa orodha yake ya wagombeaji, ilisema Bi Rwigara alifeli kutoa stakabadhi sahihi kuonyesha kuwa hajawahi kushtakiwa kwa uhalifu wowote.

Aidha, tume hiyo ilisema kuwa mwanasiasa huyo alifeli kuonyesha kuwa yuko na uungwaji wa kutosha kote nchini Rwanda kama mojawapo la hitaji la kuwania urais.

“Kuhusiana na hitaji kwamba mgombeaji aliwasilishe sahihi 600 za watu wanaomuunga mkono, alifeli kutoa angalau sahihi 12 kutoka kwa wilaya 12,” mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Oda Gasinzigwa alinukuliwa akisema.

Aidha, tume hiyo ilisema kuwa Bi Rwigara alifeli kuthibitisha kuwa yeye ni mzawa wa Rwanda.

Wakati mmoja alikuwa na uraia wa Ubelgiji lakini akauasi mnamo 2017 kabla ya kuwasilisha nia ya kuwania urais.

Lakini Bi Rwigara aliwaambia wanahabari kwamba alizaliwa Rwanda huku akipuuzilia mbali sababu zote zilizotolewa za kumzuia kuwania urais Julai mwaka huu.

Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini Rwanda ilipokea maombi kutoka watu tisa wanaotaka kuwania urais.

Orodha yake ya mwisho itatolewa Ijumaa wiki ijayo kwani tume hiyo ingali inashughulikia rufaa zilizowasilishwa kupiga hatua za mwanzo za ukaguliwa wa wagombeaji.

Hata hivyo, inasemekana kuwa muda wa Bi Rwigara kuwasilisha rufaa yake umeisha.