Habari Mseto

MKU yapokea tuzo ya hadhi ya kimataifa sambamba na Sh2 milioni

July 28th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya kimepokea tuzo ya hadhi ya kimataifa kwa kusambaza maji safi kwa mwananchi na pia kupambana na uangamizaji wa funza vijijini.

Tuzo hii inayojulikana kama ‘Tallories Network Innovative Civic Engagement Award’ na hutolewa kwa vyuo ambavyo huonyesha kujali maswala muhimu ya kijamii na maswala ya ubunifu.

Kulingana na mwenyekiti na mwanzilishi wa MKU, Profesa Simon Gicharu, chuo hicho kilipokea Sh2 milioni kutokana na tuzo hiyo.

Chuo hicho kilisambaza maji zaidi ya lita 10,000 na pia kutibu wanafunzi wa shule za msingi wapatao 1,000 waliovamiwa na funza.

Baadhi ya maeneo waliozuru kwa miradi hiyo ni kaunti za Marsabit na Kilifi.

MKU imekuwa ikijali jamii mashinani kupitia wanafunzi, wafanyakazi wa chuo na washika dau kadhaa tangu 2016.

Watu katika maeneo ya vijijini wamekuwa wakifaidika pakubwa kutokana na misaada tofauti.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Tallories Network innovative Civic Engagement, Lorlene Hoyt, alisema walitambua juhudi za MKU kutokana na kazi nzuri kinachofanya katika jamii kwa upande wa afya na maslahi mengineyo ya umuhimu katika jamii.

“Tumefurahishwa na juhudi za MKU za kujali maisha ya jamii kwa ujumla kwa kusambaza maji na kuangamiza funza. Hakika hili ni jambo la kupongezwa,” alisema Hoyt.

Kulingana na mhadhiri anayeongoza kitengo cha utafiti katika chuo hicho Dkt Peter Kirira, fedha zilizokabidhiwa chuo hicho; yaani Sh2 milioni, zitatumika kutundika vituo vya maji ya kunawa kote nchini.

“Wakati huu wa kupambana na janga la corona tunataka kukabili Covid-19 kwa kusambaza maji ya kunawa katika kila sehemu,” alisema Dkt Kirira.

Baadhi ya vyuo vingine ambayo vimeshirikiana na shirika hilo kwa juhudi za ubunifu na maswala ya kijamii ni chuo cha Cameroun, Chuo cha Nicaragua, Mexico, na kingine cha Zimbabwe.