Michezo

Mkufunzi wa zamani wa Mwamba RFC na Mean Machine ateuliwa mkurugenzi wa kiufundi katika Shirikisho la Kenya Rugby League

May 28th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Mwamba RFC na Strathmore Leos, John Mbai ameteuliwa kuwa mkurugenzi wa kiufundi wa Shirikisho la Kenya Rugby League.

Mwanaraga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya amewahi pia kudhibiti mikoba ya kikosi cha Mean Machine cha Chuo Kikuu cha Nairobi.

Katika wadhifa wake, atatakiwa kushirikiana na makocha wa vikosi vya mashinani kubuni mikakati itakayochangia makuzi ya chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji na talanta katika ulingo wa raga.

Mwenyekiti wa Kenya Rugby League, Richard Nyakwaka amesema uteuzi wa Mbai ni hatua kubwa katika maendeleo ya raga ya humu nchini.

“Analeta tajriba pevu, uzoefu wa muda mrefu na mbinu mpya zinazohitajika zaidi katika makuzi ya viwango vya raga ya humu nchini. Hapana shaka kwamba ni miongoni mwa wakufunzi wachanga ambao wana ari ya kuongoza ufufuo wa mchezo huu.”

Mbai anateuliwa siku chache baada ya mwanaraga nguli Edward Rombo kupokezwa mikoba ya ukocha wa timu ya taifa ya Kenya Rugby League.

Rombo ataongoza programu ya timu ya taifa na kushirikiana na wakfu wa Giving Rugby Foundation kupiga jeki juhudi za benchi ya kiufundi na Shirikisho la Raga la Kenya kuwakuza wanaraga wa humu nchini.

Rombo anajivunia tajriba ya takriban miaka 30 ya uchezaji na ukufunzi katika Ligi na Shirikisho la Raga.

Ndiye Mkenya wa kwanza kuwahi kusakatia kikosi cha Leeds Rugby, Dewsbury na Featherstone Rovers, Uingereza katika miaka ya 90.

Naye aliwahi kuwaongoza Mean Machine kujizolea ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya Cup mnamo 1989 na 1990 kabla ya kuchezea klabu za Watembezi Pacesetters na Barclays RFC kisha kuwa kocha wa kikosi cha Mwamba RFC.

Kibarua cha kwanza cha Mbai na Rombo kitakuwa ni kuongoza Kenya kuvaana na Afrika Kusini humu nchini katika tarehe itakayofichuliwa baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.

Mashindano ya Rugby League yaliasisiwa nchini Uingereza kabla ya kukumbatiwa nchini Australia, New Zealand na katika mengi ya mataifa barani Afrika.