Habari Mseto

Mkulima aliyeshtakiwa aokolewa na watoto mapacha

January 3rd, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MKULIMA wa mahindi katika Kaunti ya Narok anayeshtakiwa kuilaghai serikali mbolea ya bei nafuu ya Sh7 milioni, alionewa huruma na mahakama ambayo ilimuachilia kwa dhamana ndogo alipofichua mkewe alijifungua mapacha siku ile alitiwa nguvuni na polisi.

Hilary Samoei aliyeshtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi Bw Lucas Onyina, aliwakilishwa na mawakili Danstan Omari na Aranga Omaiyo.

Alipokana mashtaka mawili ya kula njama kuifilisi serikali mbolea na kudangangya alikuwa na ekari 300 anazokuza mahindi ili apewe magunia 2,398 ya mbolea, Bw Omari aliwasilisha kilio cha Samoei kwa korti.

Akasema Bw Omari: “Mshtakiwa aliye mbele yako ni maskini hohe hahe. Hana pesa nyingi kiasi cha kuweza kulipa dhamana ya pesa taslimu ya Sh1,500,000 kama washtakiwa wengine walioshtakiwa mwaka 2023.”

Akaendelea kusimulia Bw Omari: “Siku ile mkulima huyu mdogo alipokamatwa mnamo Desemba 30, 2023, mkewe alijifungua mapacha na ndiye anasubiriwa aende hospitalini kumlipia gharama ya matibabu ndipo aruhusiwe kuenda nyumbani.”

Bw Omari aliendelea kumrai hakimu amwachilie Samoei kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu ambazo watu wa familia yake wanaweza kuchanga.

Hakimu alifahamishwa na wakili kwamba zawadi ya Mwaka Mpya ambayo mahakama inaweza kumpa Samoei ni kumpunguzia dhamana “arudi nyumbani akamtoe mkewe hospitalini”.

“Mshtakiwa anafaa kupewa fursa kuwalaki mapacha katika boma lake ambapo kutakuwa na mbwembwe na raha belele,” akasema Bw Omari.

Bw Omari aliongeza kuwa “huu ni mwaka mpya na sitaki kuzugumza kwa sauti ya juu kwa vile watu wanatakiwa kuonyesha unyenyekevu na uwiano mwaka mpya”.

Wakili alimsihi kwa taadhima kuu hakimu amwachilie mshtakiwa kwa dhamana ndogo aende nyumbani kumtoa mkewe hospitalini.

Pia hakimu alielezwa kwamba mshtakiwa ndiye anayekimu mahitaji ya wazazi wake ambao ni wakongwe.

Wakili huyo aliyetoa mawasilisho kwa lugha sanifu ya Kiswahili, alimsihi hakimu aonyeshe huruma kwa mshtakiwa.

Hata Bw Omari alieleza mahakama kwamba wakili John Swaka ambaye ni mhubiri, alikuwa tayari kubariki mahakama kwa maombi na kufanya dua maalum kwa niaba ya kila mmoja mahakamani.

Akitoa uamuzi Bw Onyina alisema: “Nimesikia malilio ya Samoei kupitia kwa wakili Omari. Nimeyatilia maanani. Naamuru Samoei alipe dhamana ya pesa taslimu Sh500,000 ili aende kumnusuru mkewe kutoka hospitalini baada ya kujifungua mapacha.”

Hakimu alitenga kesi dhidi ya Samoei itajwe Januari 22, 202,  kuunganishwa na nyingine inayowakabili washtakiwa wengine watatu.

Samoei ameshtakiwa kwamba kati ya Machi 10, 2023, na Novemba 21, 202, akishirikiana na watu wengine, walikula njama za kuilaghai serikali mbolea ya bei nafuu kiasi cha magunia 2,398 ya kilo 50 kila moja.

Bei ya mbolea hiyo ni Sh7,063,000.

Shtaka la pili ni kwamba Samoei alidanganya Wizara ya Kilimo na Ustawi wa Mifugo kwamba alikuwa na shamba la ukubwa wa ekari 300 katika eneo la Olololunga, Narok Kusini ambalo ndani anakuza mahindi.

Baada ya kutoa simulizi hiyo kwa maafisa wa kilimo, Samoei alipewa magunia 2,398 ya mbolea ya bei nafuu kutumia katika ukuzaji wa mahindi ndipo bei ya unga iteremke mavuno yakitolewa shambani na kuuziwa kampuni za kusaga unga na halmashauri ya nafaka na mazao.

Kiongozi wa mashtaka alieleza hakimu kwamba mshtakiwa aliilaghai serikali mbolea hiyo.

Mshtakiwa alilipiwa dhamana hiyo ya Sh500,000 na kuruhusiwa kuenda nyumbani kumtoa mkewe kutoka katika hospitali baada ya kujifungua mapacha.