Habari Mseto

Mkulima apata maiti ya mtoto imetupwa katika shamba la mpunga

August 30th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE na MARY WANGARI

WINGU la majonzi limegubika kijiji cha Mahigaini, kaunti ya Kirinyaga baada ya mtoto mwenye umri wa miaka minne kuuawa na kutupwa katika shamba la mpunga.

Inashukiwa kwamba mtoto huyo aliyepatikana Ijumaa aliuawa kwa kunyongwa mahali kwingine na kisha kutupwa hapo ili kuficha ushahidi.

Alikuwa na majeraha kwenye shingo, ishara kwamba aliuawa kikatili na muuaji asiyejulikana kwa sababu ambazo bado hazijabainishwa.

Marehemu aligunduliwa na mkulima wa nyanya aliyekuwa ameenda kunyunyizia maji zao lake asubuhi.

Alipouona mwili huo, mkulima huyo alipiga usiahi na kuvutia umati.

Baadhi ya wanakijiji walizidiwa na hisia na kuangua kilio baada ya kumwona msichana huyo asiye na hatia akiwa amelala katika mkondo huo.

Mwanakijiji mmoja, Bw Joseph Murimi, alisema aliwahi pahala hapo pindi aliposikia kwamba mwili wa msichana ulikuwa umeonekana.

“Nilipofika hapo nilishtuka kumpata msichana huyo amefariki. Hakuweza kutambuliwa na tunashuku aliuliwa mbali na kuletwa katika kijiji chetu,” alifafanua.

Wanakijiji walitoa wito kwa polisi kuchunguza tukio hilo na kuwakamata wahusika.

“Waliotenda uhalifu huo wanapaswa kusakwa na kukamatwa ili washtakiwe,” alisema Murimi. Wanakijiji walipokuwa wakimtazama mhasiriwa, polisi waliwasili, wakauchukua mwili huo na kuupeleka katika mochari ya Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya.

Mkuu wa Polisi Mwea Mashariki, Bw John Onditi alisema uchunguzi kuhusiana na kifo cha mtoto huyo umeanzishwa.

Mauaji hayo yamejiri wiki tatu tu baada ya msichana mwingine wa umri sawa na huo kunajisiwa na kuuawa katika wadi ya Ngariama eneobunge la Gichugu.

Polisi bado hawajamkamata aliyemuua msichana huyo ambaye mjomba wake vilevile alikatwakatwa na kuuawa mwaka uliopita na kutupwa kwenye shimo karibu na kiwanda cha kahawa eneo hilo.