Makala

Mkunumbi: Kijiji cha historia ya miaka 136 kilichokataa kumalizwa na vita vya Shifta

May 10th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

KIJIJI cha Mkunumbi kina historia ndefu Lamu tangu mwaka 1888.

Wabajuni na Wasanye wengi chimbuko lao ni pale.

Kijiji hicho kilikumbwa na matatizo miaka ya sitini (1960s) wakati wa vita vya Shifta lakini kikasimama tisti bila kusambaratika.

Kwa wasiokifahamu kijiji chenyewe, Mkunumbi ni miongoni mwa vijiji asilia vya Lamu ambavyo vina ukwasi wa historia ya tangia miaka karibu 136.

Kijiji hicho kinapatikana Lamu Magharibi, ambapo ni kati ya mji wa Hindi na ule wa Mpeketoni.

Mkunumbi pia hupatikana pembezoni au kuwa karibu na barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Kihistoria, Mkunumbi ni kijiji ambacho ni makazi au ngome kuu ya Waswahili wa asili ya jamii ya Kibajuni.

Kulingana na Mwanahistoria ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee, kijiji cha Mkunumbi kilikita mizizi kuanzia mwaka 1888.

Mwanahistoria na Mzee wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee. Anasema kijiji hicho kilikita mizizi tangu mwaka 1888, wenyeji wakiwa ni Wabajuni. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hapa, Wabajuni ambao shughuli zao za kiuchumi sana sana ni uvuvi, biashara inayofungamana na masuala ya baharini, ujenzi wa mashua, jahazi, boti, kuunda nyavu na majarife, waliishi kwenye kijiji cha Mkunumbi kutokana na kwamba kimepakana na Bahari Hindi kwa upande mmoja.

Mbali na Wabajuni, jamii nyingine, ikiwemo ile ya wachache ya Boni, Wasanye na Orma pia waliishi kwenye kijiji hicho ambaco kimepakana na msitu mkuu wa Boni.

Ikumbukwe kuwa jamii ya Waboni huwa kitega uchumi chao ni kuwinda wanyama pori, kuchuma matunda ya mwituni na kuvuna asali ya mwituni.

Yaani maisha kwa jamii ya Waboni ni yale ya kimsitumsitu.

“Kijiji cha Mkunumbi kilichipuka miaka ya 1888, Wabajuni wakiwa ndio wakazi au wenyeji halisi hapa. Kwa wakati fulani Wabajuni waliungana kumpiga vita Mkoloni, hasa Wajerumani waliojaribu kuvamia na kuuteka Mkunumbi,” akasema Bw Mbwana.

Licha ya miaka mingi ya Wabajuni kujikaza na kuendelea kukisimamisha, kukinawirisha na kukitetea kijiji chao cha Mkunumbi, miaka ya sitini (1960s) ilipowadia, kijiji hicho karibu kisambaratike na kumalizwa kabisa.

Hii ni kifuatia changamoto mpya zilizozuka za kiusalama zilizochangiwa na wahalifu wa Shifta.

Vita vya genge la Shifta vilisheheni kati ya 1963 na 1967.

Bw Mbwana anasema Wabajuni wengi waliokuwa wakiishi Mkunumbi walishindwa nguvu na Shifta, hivyo kulazimisha idadi kubwa ya jamii hiyo kuhama kijijini humo na kutorokea sehemu zingine za Kenya kama vile Gongoni, Ngomeni, Malindi, Watamu na Mombasa.

Baada ya miaka mingi kupita, Wabajuni waliotoroka kutoka Mkunumbi walijenga upya mioyo na imani yao, hivyo kuanza kurudi  mmoja mmoja kuishi Mkunumbi.

Imani ya kurudi kuishi kijijini Mkunumbi pia ilijengenga na kuchochewa zaidi na kumalizika kwa vita vya Shifta.

“Leo hii ukifika Mkunumbi kweli utawapata Wabajuni ila si wengi kama ilivyokuwa awali. Wachache walirudi ilhali wengi wakiafikia kuishi walikohamia hadi wa leo kama njia mojawapo ya kujisahaulisha madhila waliyotendewa na Shifta,” akasema Bw Mbwana.

Mzee Francis Chege, ambaye pia ni Diwani wa zamani wa Mpeketoni, anasema kijiji cha Mkunumbi miaka ya sasa kimekua na kuvutia watu wa jamii tofautitofauti kutangamana na kuishi pamoja-yaani Cosmopolitan.

“Mkunumbi ya leo imechanganya makabila mbalimbali ya Kenya. Mbali na Wabajuni, utapata Wasanye, Orma, Wakore, Wasomali, Wagiriama, Wakikuyu na wengineo wakiishi pamoja. Jamii hizi zimekuwa zikitangamana au kutagusana kupitia kuoana,” akasema Bw Chege.

Ni kutokana na kukua kwa Mkunumbi ambapo wakati serikali za utawala wa magatuzi zilipochukua hatamu 2013, eneo hilo lilitengwa na kutambuliwa kuwa Wadi ya kivyake.

Isitoshe, kukua kwa Mkunumbi kulitambuliwa na serikali ya kitaifa, ambapo ni miongoni mwa tarafa mpya zilizoteuliwa na kuongezwa Lamu ili kusaidia kurahisisha utoaji huduma za serikali kwa wananchi, hasa hata wale wa mashinani kabisa.

Diwani wa Wadi ya Mkunumbi kwa sasa ni Bw Paul Kimani Njuguna ambaye pia anashikilia wadhfa wa Naibu wa Spika katika Bunge la Kaunti ya Lamu.

Sehemu mojawapo ya kijiji cha Mkunumbi kilichoko Lamu Magharibi. Kijiji hicho chenye historia ya zaidi ya miaka 100 karibu kimezwe na vita vya Shifta. PICHA | KALUME KAZUNGU