Habari za Kitaifa

Mkurugenzi na mtangazaji wa zamani Salim Swaleh alala rumande kwa kosa la ulaghai


MKURUGENZI wa Mawasiliano katika afisi ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Salim Swaleh, amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill Nairobi hadi Jumanne mahakama iamue ikiwa polisi watamzuilia kwa siku 14 wakimhoji kwa sakata ya Sh5.8milioni za ujenzi wa viwanja viwili vya michezo ya Afcon 2027.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi aliamuru Swaleh na wenzake watano Michael Otieno Japolo, Terry Kemunto Sese, Daniel Omondi Gogo, John Musundi Wabomba na James William Makoha wasalie korokoroni hadi Juni 25,2024 saa nane unusu atakapotoa uamuzi ikiwa watazuiliwa kwa siku 14.

“Ikitiliwa maanani washukiwa hawa wamefikishwa kortini saa tisa alasiri na mawasilisho ya upande wa mashtaka na mawakili wanaowatetea washukiwa hawa ni mazito, nahitaji muda kusoma na kuyatathmini yote ndipo nifikie uamuzi wa haki, washukiwa watazuiliwa kituo cha polisi cha Capitol Hill hadi Juni 25, 2024,” Bw Ekhubi alisema.

Swaleh na wenzake watano ambao ni wafanyabiashara walitiwa nguvuni Jumapili baada ya wawekezaji wawili kutoka Dubai na Afrika kusini kulalama walipunjwa Dola za Marekani (USD)45,000 (Sh5,850,000) kupewa zabuni ya ujenzi wa viwanja viwili vya michezo vya kusakatia kandanda wakati wa michezo ya Afcon 2027.

Michezo hii ya Afcon, hakimu alielezwa itachezewa nchi za Kenya,Uganda na Tanzania.

Akiomba washukiwa hawa wazuiliwe siku 14, afisa mkuu anayechunguza kesi hii Inspekta Nicholas Njoroge alisema uchunguzi wa kesi hii utatapakaa kutoka Kenya hadi Jumuia ya Milki za Uarabuni (UAE-Dubai) na Afrika Kusini.

“Mwanakandarasi mkuu aliyehusika anaishi Dubai na mwingine yuko Afrika Kusini. Itabidi polisi wasafiri hadi nchi hizo kurekodi taarifa za mashahidi. Polisi wanahitaji muda kusafiri,” Insp Njoroge alimweleza hakimu.

Ushawishi wa Salim Swaleh

Afisa huyo alisema uchunguzi huu utashirikisha idara mbali mbali za serikali kama vile Afisi ya Msajili wa Kampuni katika afisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara za Michezo, Wizara ya Usalama wa Ndani na asasi kadhaa za serikali.

“Endapo Swaleh ambaye yuko na ushawishi mkubwa ataachiliwa, atavuruga uchunguzi,” Insp Njoroge alisema huku akiomba ombi la polisi likubaliwe.

Alisema katika muda huu wa siku 14 uchunguzi wa pamoja katika mataifa hayo ya ng’ambo utafanywa kabla ya Swaleh na wenzake watano kushtakiwa rasmi.

Insp Njoroge alisema baada ya uchunguzi kukamilika washukiwa watashtakiwa kwa kula njama za kulaghai kinyume cha sheria nambari 393 za Sheria za Jinai, kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu, kutumia vibaya mamlaka ya afisi zao na kujitambua kuwa watumishi wa umma.

“Naomba polisi wakubaliwe kuwazuilia washukiwa kwa siku 14 ndipo wakamilishe uchunguzi wa kina,” kiongozi wa mashtaka James Gachoka aliomba.

Hata hivyo mawakili Shadrack Wambui, Sam Nyaberi na Danstan Omari waliomba hakimu awaachilie washukiwa hao kwa dhamana ya Sh200,000 kwa vile serikali haijawasilisha sababu tosha za kuwezesha mahakama iamuru wazuiliwe kwa siku 14.

“Insp Njoroge amekiri hana sababu maalum za kuwezesha mahakama kuagiza Swaleh na wenzake kuzuiliwa siku 14. Hakuna uhalifu umethibitishwa walifanya,” Bw Omari alisema.

Mawakili wengine Wambui na Nyamberi walisema washukiwa hawawezi kuzuilia huku polisi wakiwahoji mashahidi Dubai na Afrika Kusini.

Akisisitiza washukiwa wazuiliwe siku 14, Insp Njoroge alisema walalamishi walishawishiwa wafike katika afisi ya Mudavadi na kufanya mashauri kuhusu ujenzi wa viwanja hivi viwili.

“Baada ya kumaliza mashauri katika afisi ya Mkuu wa Mawaziri aliye pia Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni, walalamishi walifahamishwa watafululiza moja kwa moja hadi Wizara ya Usalama wa Ndani na Wizara ya Michezo. Katika kipindi hiki walalalamishi walitakiwa watoe Sh5.8m za kusajiliwa,” Insp Njoroge alisema.

Pia alisema masuala ya kidiplomasia yatahitajika katika uchunguzi huu na kwamba muda wa kutosha unahitajika.

Walalamishi hao walielezwa na washukiwa hao sita kwamba baada ya kukutana na maafisa wakuu katika wizara hizi tatu hatimaye watakutana na kufanya mashauri na Maseneta wawili ndipo zabuni yao ipate idhini kabisa.

Afisa huyo alisema Bw Swaleh aliruhusu mashauri ya mkutano na wawekezaji hao yafanywe katika afisi ya Mudavadi.

Mahakama ilielezwa Japolo alijifanya ndiye mwenyekiti wa idara ya Serikali ya uuzaji na upokeaji wa zabuni na kandarasi rasmi za serikali.

Japolo, mahakama iliambiwa, aliahidi kuharakikisha utiwaji sahihi zabuni hiyo haraka.

Hivyo basi, walalamishi walielezwa walipe USD45,000 (KSh5,850,000) ndipo washinde zabuni hiyo.

Insp Njoroge aliomba muda apate taarifa zaidi kuhusu habari za kampuni ambazo zingehusika na ujenzi huo wa viwanja kutoka Kenya, Dubai na Afrika Kusini.

[email protected]