Habari Mseto

Mkurugenzi wa kampuni ya kuuza vipande vya ardhi ashtakiwa kwa ulaghai wa Sh4.5 milioni

June 8th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa kampuni moja ya kuuza vipande vya ardhi katika Kaunti ya Kiambu ameshtakiwa kwa kupokea kwa njia ya undanganyifu Sh4.5 milioni akiwadanganya watu angewauzia raslimali hiyo eneo la Thika.

Joseph Njoroge Thuo alishtakiwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bw Daniel Ndungi pamoja na Moses Mbuchu Gikonyo.

Thuo na Mbuchu walikabiliwa na mashtaka 11 ya kupokea pesa kwa njia ya udanganyifu na kughushi hatimiliki za vipande vya ardhi katika eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu.

Thuo na Mbuchu walikabiliwa na shtaka la kupokea Sh2,250,000 kutoka kwa Bi Jane Waithera na Bi Jane Wairimu wakidai walikuwa na uwezo wa kuwauzia kipande cha ardhi ukubwa wa ekari tatu katika eneo la Countryside Coffee Gardens eneo la Kiambu.

Shtaka lilisema kuwa washtakiwa hao walikuwa wameweka tangazo katika gazeti la Daily Nation kwamba walikuwa wanauza vipande vya ardhi kupitia kwa kampuni ya Thuo Investment Company Limited (TICL).

Shtaka lilisema walipokea kitita hicho cha pesa kiasi Sh2,250,000 kati ya Mei 31, 2011, na Mei 5, 2012.

Shtaka la pili lilisema mnamo Julai 18, 2011 washtakiwa walipokea Sh1.3 milioni kutoka kwa Waithera na Wairimu wakidai wangewauzia ekari tatu za ardhi.

Septemba 28, 2011, Thuo na Mbuchu, imedaiwa walipokea tena kutoka kwa Waithera na Wairimu Sh250,000.

Tena Februari 10, 2012, washtakiwa walipokea kwa njia ya udanganyifu Sh300,000 kutoka kwa Waithera na Wairimu wakidai wangewauzia kipande cha ardhi katika eneo hilo la Countrsyide Coffee Gardens Thika, Kiambu.

Na mnamo Mei 3, 2012, washtakiwa inadaiwa walipokea Sh400,000 kutoka kwa Waithera na Wairimu wakisingizia wangewauzia ploti katika Countryside Coffee Gardens.

Mahakama imefahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba washtakiwa hao walitengeneza kwa njia isiyo halali hatimiliki za ploti na kuwapa Agnes Nyambura Maina na Mary Waithera Maina.

Cheti hicho nambari 757 kilikuwa kimetiwa sahihi na wakurugenzi wa TICL na afisa wa usorovea asiyetambulika.

Pia walishtakiwa kutengeneza cheti kingine nambari 755 kwa majina ya Agnes Wangechi na Grace Muthoni Waithaka kinyume cha sheria.

Wengine waliopokea vyeti hivyo bandia ni Agnes Nyambura Maina, Mary Waithera Kimani, Catherine Njeri Nduati, Margaret Wairimu Nduati na Antony Munyiri Kihara.

Washtakiwa walikabiliwa na shtaka la kumfuja Antony Munyiri Kihara Sh375,000 wakidai wangemuuzia ekari moja ya kipande cha ardhi eneo la Countryside Coffee Gardens, Thika, Kaunti ya Kiambu.

Mahakama iliwaachilia washtakiwa kwa dhamana ya Sh50,000 hadi Juni 25 kesi itakapotajwa tena.