Habari

Mkurugenzi wa Taj Mall atishia serikali dhidi ya kubomoa jengo

August 16th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

VITA vya ubabe vimezidi kushuhudiwa kuhusiana na shughuli ya ubomoaji wa majumba yaliyojengwa katika sehemu zisizoruhusiwa, hasa baada ya tangazo kutokea kuwa jumba la Airgate Mall (Taj Mall), jijini Nairobi ndilo litakalofuata.

Kulingana na ilani iliyotolewa Agosti 16 kutoka kwa mwenyekiti wa timu inayosimamia ubomoaji huo Moses Nyakiogora, wamiliki wa jengo hilo wametakiwa kuliondoa kabla ya Agosti 30 la sivyo libomolewe.

Kulingana na ilani hiyo, jumba hilo limejengwa katika sehemu ya barabara na hivyo kuzuia kuendelea kujengwa kwa barabara ya Outering.

“Wamiliki wametakiwa kuondoa ujenzi huo uliokiuka sheria kabla ya Agosti 30, 2018. Wapangaji wanaombwa kuondoka katika jingo hilo kabla ya muda uliotolewa kuisha,” ikasema ilani hiyo.

Ilani hiyo aidha ilisema muda uliotolewa ukiisha, jumba hilo litabomolewa kwa gharama na hasara ya wamiliki wake.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi asubuhi, Mkurugenzi Mkuu wa Taj Mall Bw Rameshchandra Govind Gorasia alitoa vitisho vikali kwa timu inayotekeleza ubomoaji wa nyumba kuwa ikiwa haitalibomoa kikamilifu hadi mchangani, wasijaribu kuliguza.

“Nataka kuomba kuwa ikiwa mnataka kulibomoa, mng’arishe kila kitu. Yeyote anayeongoza shughuli hii, ikiwa hana pesa za kulibomoa jumba hili lote asijaribu kuliguza,” akasema mmiliki huyo.

Akielekeza ujumbe wake kwa rais Uhuru Kenyatta, Bw Gorasia alisema hata ikiwa wataamua kuwa jengo hilo liko sehemu ya barabara, itakuwa bora lifanywe soko, shule ama chuo badala ya kulibomoa.

“Hii ni jasho nyingi iliyoishia katika kujenga jumba la aina hii na tuna vibali vyote vinavyohitajika, afadhali lifagiliwe lote hadi mchangani lakini lisigusweguswe na kuachwa gofu. Tusiwe na wataalamu wapumbavu,” akasema mmiliki huyo.

Alipuuzilia ilani iliyotolewa akisema haikuwa na muhuri wa kudhibitisha ni sawa, huku akifanya maombi mbele ya vyombo vya habari akimtaka mwenyezi mungu kuwachapa kiboko wale wanaowatesa watu wasio na makossa kwa kuwabomolea majumba.