Habari Mseto

Mkutano mwingine wa maombi kufanyika Murang'a

May 16th, 2019 2 min read

NDUNG’U GACHANE na CHARLES WASONGA

MKUTANO mwingine wa maombi na uzinduzi wa santuri ya video (VCD) sasa utafanyika katika uwanja wa Kimorori mjini Kenol wiki moja baada mkutano mwingine wa maombi ambao ungehudhuriwa na Naibu Rais William Ruto kuahirishwa.

Mkutano huu ambao umepangwa na msanii wa injili Martin Wa Janet utafanyika Jumapili kuanzia saa nne asubuhi.

Miongoni mwa wageni waheshimiwa ni; Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo katika Bunge la Kitaifa Bi Sabina Chege.

Bw Kuria ametangaza azma yake ya kuwania urais mnamo 2022 na pamoja na Gavana Wa Iria, viongozi hao wawili wamesajili vyama vya kisiasa ambavyo wanapanga kutumia kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022.

Wadadisi wa kisiasa wanasema hatua ya wawili hao inalenga kudhibiti umaarufu wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya.

Hata hivyo, Bw Martin Alhamisi  aliambia Taifa Leo kwamba mkutano huo sio wa kisiasa na kwamba shughuli kuu ni uzinduzi wa VCD na kuombea taifa.

Alisema aliamua mkutano huo ufanyike mjini Kenol kwa sababu unaweza kufikiwa haraka na wageni na viongozi watakaohudhuria.

Aliongeza kuwa kwa sababu amezaliwa katika kijiji cha karibu cha Kihiu Mwiri, aliamua kuandaa mkutano huo katika uwanja wa Kimorori ili watu wa familia yake na marafiki waweze kuhudhuria kwa urahisi bila kugharamika.

“Hakutakuwa na siasa wakati wa mkutano huo, ni shughuli iliyo imepangwa na waumini wa dhehebu wa Akorino kutoka kote nchini. Pia tutatumia fursa hiyo kuombea taifa kando na kuzindua VCD yangu yenye kichwa ‘Halleluiah’,” akasema.

Alipoulizwa kama amemwalika Naibu Rais katika mkutano huo, Bw Martin alisema alitaka kiongozi huyo ahudhurie lakini juhudi zake za kumfikia ziligonga mwamba.

“Nilitaka kumwalika Naibu Rais. Nilijaribu kumfikia lakini nikashindwa. Ingekuwa fahari yangu kumwona katika hafla yangu,” akasema Martin.

Alisema amepanga hafla hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu kwani hata wakati ule mkutano ambao ungehudhuriwa na Dkt Ruto ulipofutuliwa mbali, alikuwa amekodisha uwanja huo.

Mkutano wa kuzindua VCD haujawahi kufanyika katika uwanja wa Kimorori, kwani shughuli ya mwisho ya kuandaliwa hapo ilikuwa ni uzinduzi wa hospitali ya macho na meno ya Kenneth Matiba Eye and Dental Hospitali mnamo Mei 19, 2016.