Habari za Kaunti

Mkutano wa Gachagua, wafanyabiashara wadogowadogo wazaa matunda

March 29th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WAFANYABIASHARA wadogowadogo wa Nairobi wanaoagiza bidhaa kutoka ng’ambo sasa wamepata afueni baada ya serikali kuamuru bidhaa zao zinazozuiliwa katika Bandari ya Mombasa ziachiliwe ndani ya wiki mbili.

Bidhaa hizo zilizonunuliwa kutoka mataifa ya bara Asia zimezuiliwa kwa kushukiwa kuwa ghushi na kutolipiwa ushuru hitajika.

Katika mkutano ulioongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi, pia iliamuliwa kuwa ushuru wa Sh3 milioni unaotozwa kila kontena ya bidhaa, upunguzwe hadi Sh2.5 milioni.

Hii ni baada ya wafanyabiashara hao ambao ni wenye maduka katika mitaa ya Kamukunji, Nyamakima, Gikomba na Eastleigh, kulalamika kuwa Sh500,000 ziliongezwa katika ushuru huo bila wao kushauriwa.

Wengine ni wale wanaohudumu katika maeneo ya Muthurwa, Luthuli Avenue, River Road, Kirinyaga Road na eneo la katikati mwa jijini CBD.

“Naibu Rais pia alisema kuwa wafanyabiashara hao watapewa cheti kimoja cha kutimiza ubora kutoka kwa mamlaka ya kupambana na bidhaa ghushi (ACCK), Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) badala ya kila moja ya asasi hizo kuzifanyia ukaguzi bidhaa hizo na kutoa cheti,” ikasema taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo.

Kando na wawakilishi 3,000 wa wafanyabiashara hao na waagizaji bidhaa kutoka ng’ambo,  mkutano huo pia ulihudhuriwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), ACCK, na Kebs.

Wafanyabiashara hao chini ya mwavuli wa Muungano wa Wafanyabiashara wa Nairobi (NBC) wamekuwa wanalalamika kuwa wanapata hasara kutokana na masharti magumu ya ushuru na mengine ya kisheria yaliyowekwa na serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya biashara zao.

Tangu Januari 2024 wamekuwa wakilalamika kuwa bidhaa zao zinazuiliwa katika bandari ya Mombasa zikifanyiwa ukaguzi kwa kushukiwa kuwa ghushi.

Aidha, wamelalamikia hatua ya serikali kuongeza ushuru unaotozwa kila kontena ya futi 40 kutoka Sh2.5 milioni hadi Sh3 milioni.

Isitoshe, wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamikia kile wanachodai ni kunyanyaswa na maafisa wa polisi, wale wa KRA na mamlaka ya ACCK na ushindani usiofaa kutoka kwa wafanyabiashara raia wa kigeni.

Hata hivyo, nyongeza ya ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ilipitishwa na wabunge mwaka 2023 katika Sheria ya Fedha ya 2023.

Katika makubaliano yaliyosomwa na Bw Gachagua mwenyewe, ilikubaliwa kwa kuanzia sasa mamlaka ya kukapambana na bidhaa ghushi itawashirikisha wafanyabiashara hao katika mchakato wa ukaguzi wa bidhaa zao.

Aidha, ilikubaliwa kuwa KRA haitaanzisha ushuru mpya wala kupandisha kiwango cha ushuru bila kukusanya maoni kutoka kwa wadau.

“Kuanzia leo (Alhamisi) KRA itajadiliana na Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na kampuni za usafirishaji bidhaa majini kuhusu kuachiliwa kwa bidhaa zinazozuiliwa kwa sababu mbalimbali. Kuhusu kontena zilizozuiliwa, waagizaJI bidhaa watalipa ushuru hitajika na KRA itaziachiliwa kwa wenyewe,” Bw Gachagua akasema.