Habari MsetoSiasa

Mkutano wa Raila wachemsha siasa Bonde la Ufa

April 14th, 2019 2 min read

WYCLIFF KIPSANG na BARNABAS BII

MKUTANO baina ya kiongozi wa Upinzani Raila Odinga na baadhi ya viongozi wa Bonde la Ufa umezua joto la kisiasa katika eneo hilo.

Baadhi ya wanasiasa sasa wanasema mkutano huo wa Bw Odinga unalenga kugawanya kura za Bonde la Ufa hivyo kusambaratisha ndoto ya Naibu wa Rais William Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono amewashutumu wanasiasa waliokutana na Bw Odinga akisema kwamba walifanya hivyo kwa masilahi yao binafsi.

“Hawa watu waliokutana na Bw Odinga hawakutumwa na wakazi wa Bonde la Ufa kwani hawakuchaguliwa. Hawana usemi katika siasa za jamii ya Wakalenjin na wanafahamika kwa kuwa waasi,” akasema Bw Rono ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Viongozi kutoka Bonde la Ufa waliokutana na Bw Odinga walisema kuwa wanaunga mkono ‘handisheki’ baina yake na Rais Kenyatta.bonde

Miongoni mwa viongozi waliokutana na Bw Odinga ni mbunge Maalumu Wilson Sossion, aliyekuwa mbungerift maalumu Musa Sirma, Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat na wanasiasa David Koech, Lucas Chepkitony, Paul Sang, Micah Kigen na Kipkorir arap Menjo.

Wakizungumza wakati wa mkutano huo, viongozi hao wa Bonde la Ufa walitaka miradi yote ya maendeleo katika eneo hilo ikaguliwe ili kuthibitisha ikiwa utaratibu wa kutoa kandarasi ulifuatwa au la.

Wanasiasa hao walimtaka Rais Kenyatta na Bw Odinga kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na wakawataka wakamate washukiwa wa wizi wa fedha za umma.

Kulingana na Bw Kigen, kiongozi wa ODM katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, mkutano huo haukuwa na uhusiano na siasa za 2022.

“Tutaendelea kuandaa mikutano zaidi na Rais Kenyatta pamoja na Bw Odinga ili kutafutia ufumbuzi changamoto zinazokumba kilimo, maziwa, majani chai kati ya sekta nyinginezo,” akasema Bw Kigen.

Alisema mkutano mwingine sawa na huo unatarajiwa kufanyika mwezi ujao na utajumuisha wawakilishi wa wazee, viongozi wa makanisa, vijana na akina mama.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany alishutumu mkutano huo akisema kuwa viongozi hao wamepoteza mwelekeo.

“Wanafaa kutangaza wazi kwamba wanaunga mkono Bw Odinga katika kinyan’ganyiro cha 2022 na kufanyika kwa kura ya maamuzi,” akasema Bw Kositany, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.