Habari MsetoSiasa

Mkutano wa Ruto Murang’a waahirishwa ghafla

April 25th, 2019 3 min read

NA NDUNGU GACHANE

MKUTANO mkubwa wa maombi uliopangiwa kufanyika Jumamosi mjini Kenol katika Kaunti ya Murang’a, ambapo Naibu Rais William Ruto alipangiwa kuhudhuria umeahirishwa ghafla baada ya migawanyiko kuibuka miongoni mwa maaskofu waandalizi.

Mkutano huo sasa umepangiwa kufanyika mnamo Mei 11.

Kulingana na mwenyekiti wa maaskofu hao, Bw Stephen Maina , wa kanisa la Full Time Winners Gospel Church, mkutano huo uliahirishwa baada ya kubainika kwamba Dkt Ruto atakuwa akihudhuria mazishi ya Jonathan Moi, ambaye ni mwanawe Rais Mstaafu Daniel Moi.

“Dkt Ruto hatakuwepo kwani atakuwa akihudhuria mazishi ya mwanawe Mzee Moi. Tumeamua kuuahirisha kwani ndiye aliyekuwa mgeni wa heshima,” akasema kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Mnamo Jumatano, askofu huyo alisema mkutano huo ulipangwa na maaskofu 11 ambao walitarajiwa kukutana na Dkt Ruto katika hoteli moja kabla ya kuelekea katika uwanja wa Kimorori, ambako mkutano huo ungeandaliwa.

Kulingana na Bw Maina, kamati andalizi inajumuisha Askofu wa Dayosisi ya Murang’a ya Kanisa Katoliki James Wainaina, maaskofu Timothy Gichere wa kanisa la ACK katika Dayosisi ya Mlima Kenya ya Kati, Julius wa Dayosisi ya Murang’a Kusini Julius Karanu, Julius Wanyoike wa Dayosisi ya Thika, Askofu Gilbert Maina wa kanisa la EAPC, John Mwati wa kanisa la PCEA kati ya wengine.

Alisema kwa baadhi ya mambo yaliyopangiwa kuombewa ni utangamano wa kitaifa, na kumwombea Dkt Ruto, ambaye amekuwa akielekezewa lawama bila sababu zozote.

Hata hivyo, mgawanyiko mkubwa ulidhihirika miongoni mwa viongozi hao, ambapo Askofu Wainaina wa Kanisa Katoliki akisema kuwa ingawa alikuwa akifahamu kuhusu uwepo wa mkutano huo, hakuhudhuria mikutano hiyo na hakuwa akipanga kuhudhuria kwani atakuwa na shughuli zingine.

“Ukweli ni kuwa, ingawa nilikuwa nikifahamu uwepo wa mkutano huo, sijawahi kushiriki katika kikao chochote cha maandalizi yake. Sipangi kuhudhuria kwani nina mipango mingine,” akasema, kwenye mahojiamo.

Hata hivyo, Dkt George Kariuki wa kanisa la Christian Foundation Fellowship (CFF) alisema kuwa huenda migawanyiko hiyo imesababishwa na mdahalo ulioibuka majuzi kuhusu michango ya Dkt Ruto katika makanisa.

Alisema kuwa mkutano huo ulipangwa tangu mwaka uliopita na zaidi ya viongozi wa kidini 250 ambao walimtembelea Dkt Ruto katika makazi yake ya Karen.

Chama maalum cha ushirika pia kilipangiwa kuzinduliwa.

Viongozi waliotarajiwa kuhudhuria ni Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, wabunge Mary Waithera (Maragua), Alice Wahome (Kandara) na viongozi zaidi ya 150 wanaomuunga mkono Dkt Ruto.

Kwengineko, Mkurugenzi wa jinai (DCI) George Kinoti amefichua kuwa wizi uliotekelezwa katika mashine nne za kutoa pesa (ATM) za benki ya Barclays ulihusisha wafanyakazi wa ndani.

Alieleza jana kuwa uchunguzi kuhusiana na wizi huo ambapo Sh14 milioni ziliibwa upo karibu kumalizika.

Akizungumza katika afisi kuu za polisi kanda ya Pwani jijini Mombasa, Bw Kinoti alisema kuwa visa hivyo vilikuwa vimepangwa na “watu wao wa ndani”.

“Walijua kitu ambacho kilikuwa kinafanyika. Huku nje ilikuwa ni watu tu wa kutekeleza yale yaliotakiwa na njia ya kupata pesa hizo ili waweze kugawana baadaye. Lakini tutaweka wazi ili umma uone,” akasema Bw Kinoti ambaye alikuwa ameandamana na Mkurugenzi wa Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji

Bw Kinoti alisema kuwa kulingana na matukio hayo, inaaminika kuwa kulikuwa na mtu ambaye alikuwa ameekwa akitizama kamera za CCTV wakati majambazi hao walikuwa wakitekeleza wizi huo.

Alisema kuwa kulingana na kile kilichokuwa kimelengwa na wezi hao, ni wazi walikuwa na mtu anayewasaidia kutoka ndani.

“Sijui tuite huu wizi ama nini. Lakini kwa ukweli ni kuwa kulikuwa na mtu anahusika kutoka ndani. Sitoweza kusema mengi kwa sababu uchunguzi bado unaendelea lakini tutaweka bayana yale yaliotukia ili kampuni nyengine ziweze kuona na kujifunza,” akasema.

Bw Kinoti alisema kuwa kesi hiyo hivi karibuni itafikishiwa Bw Haji ili wahusika wafikishwe mahakamani.

“Tupo karibu kumaliza uchunguzi. Na tutapeana ripoti ya uhakika kwa DPP na kile ninachomuomba ni ahakikishe kuwa kesi hii inachukuliwa kwa umuhimu mkubwa,” akasema Bw Kinoti.

Alisema kuwa washukiwa wa kutosha wametiwa mbaroni kuhusiana na kesi hiyo na kueleza kuwa wengine watakamatwa.

Alipoulizwa na Taifa Leo kuhusiana na idadi ya waliokamatwa, Bw Kinoti aliongeza kuwa: “Kesi bado ipo kwenye uchunguzi lakini cha uhakika ni kuwa tuko na washukiwa wa kutosha ba tutashika wengine. Niko na Imani tutashika wengi zaidi.”

Miongoni mwa wale waliokamatwa kufikia sasa ni wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya G4S.

Watano hao walikamatwa mnamo Jumatatu eneo la Kenya Cinema barabara ya Mama Ngina ambapo wizi huo uliripotiwa kufanyika.