Habari Mseto

Mkutano wa waathiriwa wa 2007/8 watibuka makundi mawili yakipigania fidia

April 15th, 2019 1 min read

RICHARD MAOSI NA KEVIN ROTICH

MKUTANO wa waathiriwa wa ghasia za uchaguzi wa 2007/8 ulioratibiwa kufanyika uwanjani Afraha Jumatatu ulitibuka kutokana na mizozo ya uongozi.

Hafla hiyo ilipania kumshukuru Rais Uhuru Kenyatta baada ya kuwafidia wakati walikuwa karibu kukata tamaa maishani.

Kulingana na msemaji wao James Maina, wamekuwa wakilalamikia haki yao kwa muda mrefu hadi rais aliposikia malilio yao na kutoa msaada.

Aidha kumekuwa na mzozo baina ya viongozi wa kundi la waathiriwa huku mirengo miwili iking’ang’ania kuendesha ugavi wa fedha.

“Tulikuwa tumechoka na uongozi wa Patrick Githinji aliyekuwa amefuja hela, ndipo tukamteua Margaret Gathoni kama mwenyekiti mpya,” alisema.

Alisema pesa za walioaga dunia zilizoingia kwenye akaunti ya Equity tawi la Kitale zilikuwa zimehamishiwa kwa akaunti za watu tofauti.

Inadaiwa Bw Patrick Githinji amekuwa akiwalipa watu wasiostahili kupata fidia kutoka kwa serikali.

Mwathiriwa huyu wa uchaguzi wa 2007 alitazama tu kwa umbali asijue la kufanya. Picha/Richard Maosi

Kwa upande mwingine aliongezea kuwa Bi Margaret alipata kibali kutoka kwenye kituo cha polisi cha Bondeni kuendesha mkutano huo.

Mkutano ulianza asubuhi lakini mwendo wa saa sita Bi Margret alikamatwa na kuzuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Bondeni akisubiri kufikishwa mahakamani.

Peter Etan mwanachama wa National IDPs Network alisema kuwa upande unaomuunga mkono Bw Patrick ulikuwa na njama ya kuchukua uongozi kwa lazima.

“Waathiriwa 18 kutoka kaunti ya Turkana mpaka sasa hawajapokea fidia na huenda pesa zimeingia kwenye mifuko ya watu wachache,” akasema.

OCPD wa Nakuru Bi Hellen Wairimu alikinzana na madai hayo akisema mkutano huo haukuwa umeidhinishwa na serikali ya Kaunti ya Nakuru.

“Bi Margret alikuwa akutane na kamishna wa kaunti ya Nakuru kujadili masaibu yanayowakumba waathiriwa, lakini akasusia mkutano na kuwatuma watu wengine,” alisema

Atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kwa kukaidi agizo na kuendesha mkutano bila kibali.