Habari MsetoSiasa

Mkutano wapangwa kuunganisha viongozi wa Pwani

March 26th, 2018 2 min read

Waziri msaidizi wa Wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro. Picha/ Maktaba

NaMOHAMED AHMED

VIONGOZI wa Pwani wanapanga kukutana kujadili masuala yatakayowaunganisha, Waziri msaidizi wa wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro amesema.

Bw Mung’aro alisema kuwa mwezi ujao viongozi wote wa kutoka pwani watakutana katika kaunti ya Kwale ili kujua mustakabali wa eneo hilo.

Akizungumza wakati wa mazishi ya mke wa aliyekuwa waziri wa utalii marehemu Karisa Maitha, Bi Alice Maitha mnamo Jumamosi, Bw Mung’aro alisema kuwa mkutano huo unatazamiwa kuunganisha viongozi hao kwa ajili ya matakwa ya mpwani.

“Tusifurahie kukutana kwa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga. Inafaa sisi wenyewe kama viongozi tusalimiane ndio tujue kuwa kweli tumeungana. Tunafaa kufurahia pia tukiona Mung’aro, Joho na Kingi wanasalimiana,” akasema Bw Mung’aro.

Bw Mung’aro ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Kilifi Kaskazini alizungumzia muungano huo baada ya viongozi wa kaunti hiyo ya Kilifi na Mombasa kueleza kuwa kuna haja ya kuungana kama Wapwani.

Naibu gavana wa Mombasa William Kingi alisema kuwa kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga ni “fursa nzuri kwa Wakenya na kwa Wapwani”.

“Inapaswa tutumie fursa hii kuendesha mambo yetu mbele. Sisi kama Wapwani tuna kila sababu ya kutumia nafasi hii kuona tunaungana ili tuweze kutambulika nafasi yetu kitaifa,” akasema Dkt Kingi.

Naibu gavana wa Kilifi Gideon Saburi alisema kuna haja ya wakazi wa Pwani na viongozi kuwa kitu kimoja ili waweze kutatua matatizo yao na yaweze kusikizwa katika mazungumzo ya kitaifa ambayo yanapaswa kufanyika kufuatia kuungana kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Mbunge wa Kaloleni Paul Katana alisema kuwa kuna haja ya kuungana kwa Wapwani kwa sababu ya maendeleo ya eneo hilo.

“Sisi tutafuata hatua zile zile kama za Baba za kuunganisha Wakenya. Na sisi kama Wapwani lazima tushikane ili tulete maendeleo kwa watu na bila hivyo hatuwezi faidika,” akasema Bw Katana.

Mbunge wa eneo bunge la Kilifi Kusini Ken Chonga alisema kuwa mazungumzo ya kutaka kuungana kwa Wapwani yamekuwa kwa muda na kuongeza kuwa hilo litafanyika wakati Wapwani wataunda chama chao.