Habari Mseto

Mkuu wa ATPU aamriwa kufika kortini

June 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA anayesimamia kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi (ATPU)  Alhamisi aliamriwa afike kortini kueleza sababu ya kutowaachilia washukiwa watano wa ugaidi.

Hakimu mwandamizi alitoa agizo hilo baada ya kufahamishwa na wakili Albert Makori kuwa “ Polisi wamekaidi agizo lake.”

“Polisi wa kitengo cha ATPU wamekataa kuwaachilia washukiwa watano wa ugaidi ambao wamekaa rumande mwezi mmoja sasa,” alisema Bw Makori.

Bw Makori alisema polisi hawakuwapata na hatia washukiwa hao Mabw Abdi Aziz Bule Ali, Abey Rashid Ibrahim,Hassan Osman Mohamud  Abdirahaman , Bashir Mohammed na Qadro Jamal Gaite na wamekataa kuwaachilia kinyume cha sheria.

Bi Mutuku aliamuru Juni 18 washukiwa hawa waachiliwe huru lakini polisi wanaendelea kuwazuilia.

“Naomba hii mahakama iamuru msimamizi wa ATPU afike kortini kueleza sababu ya kukaidi maagizo ya mahakama,” Bw Makori alimweleza hakimu.