Habari Mseto

Mkuu wa Kerra ashurutishwa kulipa wakulima Sh163 milioni

July 18th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilimwamuru mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya kitaifa ya ujenzi wa barabara (KERRA) Bw Luka K Kimeli awalipe wakulima 41 zaidi ya Sh163 milioni kwa kunyakua mashamba yao kujenga barabara ya Gikambura-Thogoto-Mutarakwa.

Na wakati huo huo Jaji Kossy Bor alimwagiza Bw Kimeli amlipe wakili Jeremy Njenga Sh11milioni katika muda wa siku 30.

Jaji Bor alitoa agizo hilo baada ya Bw Kimeli kufika kortini kueleza sababu hawezi kusukumwa ndani kwa kukaidi agizo la korti amlipe Bw Njenga pesa kwa kuwatetea wakulima hao ambao mashamba yao yalitwaliwa bila idhini yao.

Mahakama ilikuwa imeelezwa kuwa Bw Kimeli amekataa kumlipa Bw Njenga pesa hizo.

“Mimi sijakataa kumlipa Bw Njenga pesa hizi. Tayari nimewalipa wakulima ambao mashamba yao yalichukuliwa na barabara kuengwa. Kwa upande wa wakili huyu sijui nimlipe nani,” alisema Bw Kimeli kupitia kwa wakili Bw Mwangi Wahome.

Bw Wahome alisema kuwa pesa za umma hazipasi kutupwa mbali zahitaji kutumika kwa njia ifaayo.

Baada ya kupokea hakilkisho kuwa pesa hizo zitalipwa basi Jaji Bor alimwamuru mkurugenzi huo mkuu alipe pesa hizo katika muda wa siku 30.

Wakulima hao waliwasilisha kesi mnamo 2014 dhidi ya KERRA, tume ya kitaifa ya ardhi (NLC) na wizara ya ardhi wakiomba washtakiwa washurutishwe kuwalipa fidia kwa kunyakua mashamba yao kujenga barabara.

Walalamishi walisema kuwa mashamba yao yalitwaliwa mwaka wa 2010-2011 na KERRA kujenga barabara.

Bw Njenga aliyewatetea walalamishi alisema kuwa washtakiwa waliingilia mashamba yao na hawakuwalipa fidia.

Waliiomba mahakama itangaze hatua hiyo ya Kerra kuruhusu makampuni ya kujenga barabara ya Kudhan Singh na Victoria Construction Co. Ltdm ilikandamiza haki zao.

Jaji Bor alikubaliana na wakili Njenga kuwa haki za wakulima hao zilikandamizwa na kwamba wanapaswa kulipa fidia.

Wakili alisema kuwa wizara ya ardhi haikuchapisha katika gazeti rasmi ya Serikali kwamba mashamba ya wakulima hao yatatwaliwa kujenga barabara ya Gikambura-Thogoto-Mutarakwa katika kaunti ya Kiambu.

Mahakama iliamuru wakulima hao walipwe zaidi ya Sh163milioni kama fidia na Bw Njenga alipwe Sh11milioni ikiwa ni gharama za kesi.

Alipokataa kulipa pesa hizo , Bw Njenga aliomba Jaji Bor amsukume jela Bw Kimeli kwa kukaidi agizo la mahakama.

NLC iliamuru wizara ya ardhi iwalipe wakulima pesa hizo.

“Maagizo ya mahakama hayatolewi bure tu. Lazima yatekelezwe,” Nw Njenga alimweleza Jaji Bor.

Jaji Bor alikubaliana na wakili Njenga na kuamuru Kerra kupitia kwa Bw Kimeli ilipe pesa hizo.