Kimataifa

Mkuu wa wafanyakazi White House augua Covid-19

November 7th, 2020 1 min read

Na AFP

WASHINGTON D.C., Amerika

MKUU wa wafanyakazi katika Afisi ya Rais wa Amerika Donald Trump Mark Meadows amethibitishwa kuwa na Covid-19, vyombo vya habari nchini Amerika vimeripoti.

Meadows, 61, aliwaambia watu kuwa ana virusi vya corona baada ya kukamilisha kwa shughuli ya upigaji kura katika uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba 3, 2020, shirika la habari la CNN liliripoti.

Alipatikana na virusi hivyo Jumatano, siku moja baada ya uchaguzi huo, kulingana na gazeti la New York Times.

“Meadows alisema ni miongoni mwa umati wa watu waliokuwa katika Ikulu ya White House Jumatano asubuhi waliomsikiza Rais Trump akiwahutubia kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi huo,” gazeti la Washington Post liliripoti.

Maafisa kadhaa wa ngazi za juu katika serikali ya Trump wamepatikana na virusi vya corona katika majuma machache yaliyopita, akiwemo mke wa Rais huyu Melania Trump.

Katibu wa mawasiliano Kayleigh McEnany na washauri wa masuala ya sera Stephen Miller na Hope Hicks ni miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi ya juu katika Ikulu ya White House ambao wameambukizwa virusi vya corona ndani ya mwezi wa Oktoba.