Habari Mseto

Mlanguzi wa mihadarati atiwa nguvuni Murang'a

August 15th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MAAFISA wa polisi katika Kaunti ya Murang’a wakiwa katika harakati za kuwaandama walanguzi wa mihadarati ambao wanauzia watoto wa shule walio nyumbani kwa sababu ya Covid-19 wamemtia nguvuni kiongozi wa biashara hiyo haramu katika Mji wa Kenol.

Maafisa hao wametumia ubunifu wa kumtumia mwanafuzni wa kidato cha tatu ambaye usiku wa kuamkia jana Ijumaa alikuwa amenaswa akivuta bangi na katika ile hali ya uchunguzi, maafisa wakamtumia kumtia mbaroni mlanguzi huyo kwa jina Laurence Mwangi Mureithi.

Inadaiwa mhalifu amekuwa katika biashara hii haramu kwa kipindi cha miaka 12 hadi sasa katika mji huo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Anthony Keter, mwanafunzi huyo alitiwa mbaroni lakini maafisa wakaona busara imo katika kumsaka aliyemuuzia.

“Mwanafunzi alikubali kushirikiana na maafisa na kwa kuwa alikuwa na nambari ya simu ya mlanguzi huyo, alitumiwa kumpigia akisingizia kutaka mihadarati zaidi kwa nia ya kumvuta hadi kwa mtego wa maafisa,” akasema Bw Keter.

Bw Keter alisema ubunifu huo ulifanikiwa kumleta mlanguzi huyo hadi kwa mtego wa polisi na baada ya kukamatwa akaelekeza maafisa hadi nyumbani kwake ambapo kulitekelezwa upekuzi uliozaa matunda.

“Tumepata kilo 15 za bhangi ambayo haijaandaliwa kwa soko, misokoto 250 ya bidhaa hiyo tayari kwa soko, lita 50 za pombe ya kitamaduni aina ya Muratina, karatasi spesheli inayotumika kufunga bangi; bidhaa hizi zote zikiwa za thamani ya Sh200,000,” akasema.

Bw Keter alisema kuwa Rais Uhuru Kenyatta ameamrisha vitengo vyote vya maafisa wa usalama viwaandame wote ambao wanashiriki vitendo vya kuhujumu maadili ya watoto katika jamii na “wakinaswa waorodheshwe kama maadui wa kitaifa ambao wanalenga kudhalalisha kesho ya watoto na taifa kwa ujumla.”

Alisema kuwa wote ambao wanashiriki biashara za kuwapa wanafunzi mihadarati katika eneo hilo waelewe kuwa mkono wa sheria unawaandama kwa dhati.

“Tukiongozwa na wakuu wakubwa wetu wa usalama wa Kaunti, tumejumuishwa katika amri ya kuwajibikia kero hili na Kamishna wetu Mohammed Barre pamoja na Kamanda wetu wa Polisi Bw Josephat Kinyua na kamati zote za kiusalama kwa pamoja tumeamua hivi ni vita tutaendeleza hadi mwisho wake,” akasema.