Dondoo

Mlevi aokoka kwa kunusurika kifo

January 13th, 2020 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

CHEPALUNGU, BOMET

KULIKUWA na kioja eneo hili mlevi alipozuru mtaro mmoja hatari ambao alikuwa ametumbukia usiku uliotangulia na kupiga magoti kuomba kushukuru Mola kwa kumuokoa.

Kulingana na duru za meza ya dondoo, jombi aliacha kushiriki kanisa miaka kadhaa iliyopita na akaanza kupiga mtindi kinyume na ushauri kutoka jamaa na marafiki.

“Alianza kunywa pombe kwa njia ya kushangaza kwani alilewa chakari na hata kukesha njiani bila kufika kwake. Wakati mwingine alikuwa mwenye fujo sana,” mdaku alieleza.

Juzi, alielekea mangweni na kuitisha dozi kama kawaida yake na usiku ulipoingia mama pima akamsukuma nje kwa kuwa alitaka hata naye apumzike.

” Nje, jamaa alikabiliwa na mvua tele na akajikokota kuelekea nyumbani kwenye giza totoro akiwa amelowa maji,” mdokezi alisimulia.

Asubuhi, jamaa alijipata kwake akiwa hoi na akamtaka mkewe amweleze alivyofika nyumbani usiku wa manane.

” Shukuru Maulana maana ulianguka kwenye mtaro hatari na wapita njia wakakuokoa na kukuleta hadi hapa. Okoka tena sasa maana umepata ushuhuda wa kutosha kuwa Mungu bado anakuthamini,” mkewe alimweleza mumewe.

Moja kwa moja jamaa alishika njia kuona mtaro mkubwa aliotumbukia usiku na alipofika akashika tama kujua aliponea kwa tundu la sindano.

“Ghafla jamaa alipiga magoti na kutoa sala ya kipekee kushukuru kwa Mola kwa kumlinda huku akiahidi kurudi kumtumikia tena,” mdokezi akatuarifu.

Wapita njia walikatiza safari kufuatilia tukio hilo lakini jamaa hakuogopa chochote na akaendelea kuomba.

Alipomaliza, alianza safari kuelekea kwa pasta wake wa awali kutangaza amerudi kuwa kondoo wake tena.