Kimataifa

Mlevi aua mamake kwa kutomwandalia kitoweo cha kuku

June 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

GUNTUR, INDIA

MWANAMUME mlevi alimuua mamake mkongwe kwa sababu hakupika kitoweo cha kuku wakati wa chakula cha mchana.

Tukio hilo liliwashangaza wengi katika eneo la Badepuram, Wilaya ya Guntur ambao walifichua mwanamume huyo aliyetambuliwa kama Bejjam Kishore, 45, alikuwa ni mnywaji pombe kupita kiasi.

Ilisemekana Kishore alikuwa ni afisa wa matibabu katika maeneo ya mashambani na alikuwa na tabia ya kunywa pombe kila siku, hali iliyomfanya mke wake kumtoroka miaka kadhaa iliyopita.

Kulingana na mashirika ya habari, mwanamume huyo alinunua kuku asubuhi akampelekea mamake, Bejjam Mariamma, 80, ili apike kitoweo cha chakula cha mchana.

Lakini Kishore aliporudi nyumbani kutoka ulevini, alikuta mamake hajapika kuku ndipo akachukua kisu na kumdunga akafariki papo hapo.

Ripoti zinasema majirani waliosikia kilio cha mwanamke huyo walikimbia nyumbani kwake lakini wakakuta mshukiwa alikuwa ametoroka. Walipiga ripoti kwa polisi ambao walianzisha msako kumtafuta ili ashtakiwe.

-Imekusanywa na Valentine Obara