Dondoo

Mlevi avisha kisura wa baa pete

December 12th, 2020 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

NGOLIBA, KIAMBU

MLOFA aliyekuwa akiburudika katika kilabu kimoja mtaani hapa aliwachekesha wenzake alipoamua kumvisha pete mhudumu wa kilabu hicho aliyempapasa.

Jamaa alidai tangu alipoanza kuwa na uhusiano na wanawake, hakuwa amepata aliye stadi wa kupapasa madume kama mwanadada huyo.

“Katika maisha yangu, sijawahi kuhisi nilivyohisi mwanadada huyu aliponipapasa,” jamaa alisema bila kufafanua.

Inasemekana jamaa alisimama mbele ya wateja wengine, akamkumbatia demu huyo na kumpiga mabusu moto moto kabla ya kutoa pete na kutaka kumvisha. Huku wateja wakidhani jamaa alikuwa akifanya mzaha, demu alikubali kuvishwa pete.

“Kuanzia leo hautafanya kazi katika kilabu hiki. Ulifanya kitu ambacho sijawahi kufanyiwa na mwanamke mwingine. Ulinipapasa nikahisi vizuri kuliko ninavyohisi nikipapaswa na wanawake wengine. Kwa hivyo nitakuvisha pete mbele ya watu hawa kwa sababu tayari nimekupenda,” jamaa alisema.

Inasemekana watu kilabuni walishangilia kwa shangwe na nderemo mwanadada alipokubali pete hiyo. “Wanawake wengine wangekuwa sampuli yako ningekuwa ninahisi vizuri. Sasa wengine wanaonimezea mate watajipanga. Nitakuoa uwe mke wangu na nitakutunza vizuri,” jamaa aliongeza.

Inasemekana demu alidondokwa na machozi ya furaha huku wateja wakipigwa na mshangao.

“Mungu ni wa maajabu. Nimeishi kwa miaka mingi na hakuna mwanamume aliyejitolea kunivisha pete. Nioe tu hata kama una mke mwingine sitajali,” demu alisema.

Yadaiwa jamaa alifurahi sana mpaka akawanunulia watu waliokuwa karibu na meza yake pombe. Ilibainika kuwa wawili hao walikuwa wamekula ufuska kwa muda kabla ya tukio hilo.

Hata hivyo haikujulikana iwapo uhusiano wa wawili hao uliendelea baada ya kioja hicho.