Dondoo

Mlevi azua kioja kwa baa kudai mteja ni mkewe

April 12th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA 

GATUNDU, KIAMBU

Polo mmoja alizua kioja kwenye baa baada ya kulewa na kudai kuwa mrembo aliyeketi na jamaa fulani karibu naye alikuwa mpenzi wake.

Kulingana na mdokezi, polo akiwa na wenzake waliingia baa na kuitisha vinywaji. Muda mfupi baadaye kalameni fulani aliingia akiandamana na mrembo wake na wakaitisha vinywaji pia.

Duru zinasema baada ya mafunda kadhaa polo aliinuka taratibu na kuelekea alikokuwa ameketi kalameni aliyeingia akiwa na mrembo. “Boss huyu ni mpenzi wangu. Umemtoa wapi,” polo alimueleza jamaa yule huku akimshika mrembo mkono.

Jamaa alimuangalia polo kwa mshangao.  “Mimi sikujui. Nenda zako,” mrembo alimkemea polo huku akimsukuma.

Jamaa alisimama pale na kuanza kumlazimisha mrembo aandamane naye hadi alikokuwa ameketi. “Wewe acha zako. Nakujua. Wewe ni mchumba wangu.Tulikutana nawe mwezi uliopita sokoni,” polo alimueleza mrembo.

Kulingana na mdokezi, kipusa alipigwa na butwaa aliposikia madai ya polo. Marafiki wa polo walianza kuangua vicheko. “Huyu pombe imemuweza. Tusimruhusu anywe tena. Ameanza kuwasumbua watu,” walisikika wakisema.

Jamaa aliyekuwa ameandamana na mrembo aliinuka na kumuondoa polo mbele yake. “Toka hapa haraka. Peleka ulevi wako kule. Huyu ni mke wangu,” jamaa alimfokea polo.

Polo hakuwa na jingine ila kurejea walikokuwa marafiki zake. “Wewe una shida gani? Huyo demu ni wa huyo jamaa. Kwani umelewa hadi huwezi kumtambua mchumba wako?” polo aliulizwa na rafiki yake mmoja.

Jamaa hakusema lolote. Wenzake walibaki kumcheka. “Kuanzia kesho ukija kulewa, hakikisha unaandamana na mrembo wako. Haya mambo ya kurukia mademu wa wenyewe komesha,” polo alikemewa na wenzake.

…WAZO BONZO…