Mlima Kenya ‘kuwatahini’ wawaniaji wa urais 2022

Mlima Kenya ‘kuwatahini’ wawaniaji wa urais 2022

Na MACHARIA MWANGI

VIONGOZI wa Mlima Kenya wataandaa orodha ya maswali watakayotumia kuwapiga msasa wawaniaji wa urais kabla ya kutangaza msimamo kuhusu watakayemuunga mkono mwaka 2022.

Viongozi hao wa vuguvugu la Mt Kenya Unity Forum, wakiongozwa na kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua, Jumatatu walisema maswali hayo yanaangazia masuala manne makuu ambayo ni muhimu kwa ustawi wa eneo la Mlima Kenya.

Bi Karua alisema kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto tele huku akitoa mfano wa Kaunti ya Laikipia ambayo inakumbwa na tatizo la ukosefu wa usalama.

“Usalama pia ni suala muhimu ambalo tunahitaji lishughulikiwe haraka na serikali,” akasema Bi Karua.

Alishikilia kwamba suala la ugavi wa rasilimali kwa usawa na uwakilishi linahitaji kushughulikiwa.

Alisema vuguvugu hilo pia linatetea demokrasia ya vyama vingi nchini.

Bi Karua ameteuliwa kuwa msemaji wa vuguvugu hilo linalojumuisha viongozi ambao wamekwama kisiasa katikati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto.

“Lengo letu kuu ni kuunganisha eneo la Mlima Kenya hata baada ya uchaguzi mkuu ujao,” akasema waziri huyo wa zamani wa Haki.

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo alisema kuwa hawatalegeza kamba katika juhudi zao za kutaka kuunganisha eneo la Mlima Kenya.

“Masilahi ya eneo la Mlima Kenya ndio tunatetea. Tunakaribisha kila mtu kujiunga na vuguvugu hili,” akasema Bw Kabogo.

Aliyekuwa waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye pia ni kiongozi wa The Service Party, alisema viongozi wa Mlima Kenya wako huru kujadili masuala nyeti yanayoathiri watu wa eneo hilo bila uwoga.

Mbunge wa zamani wa Subukia Koigi wa Mwere alisema kuwa viongozi hao wameungana kuhakikisha kuwa jamii za Mlima Kenya zinazungumza kwa sauti moja.

You can share this post!

Koeman achemkia wanahabari kwa kuuliza mustakabali wake...

Rais Hichilema asifiwa kwa kutumia ndege ya abiria ziarani...