Siasa

Mlima Kenya: Mwindaji wa kisiasa anayekosa ‘mbwa kiongozi’

January 5th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

WAKATI Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta aliondoka uongozini Septemba 2022, mojawapo ya maswali yaliyoibuka ni kuhusu yule ambaye angekuwa kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda wa Mlima Kenya.

Machoni mwa wengi, Naibu Rais Rigathi Gachagua, bila shaka ndiye aliyeonekana kuwa mrithi wa Bw Kenyatta, kwani hadi sasa, ndiye mwanasiasa anayeshikilia nafasi ya juu zaidi katika serikali ya Kenya Kwanza.

Katika harakati za kujaza pengo la Bw Kenyatta, Bw Gachagua alianza kwa kufanya mikutano katika sehemu tofauti eneo hilo, akiwashukuru wenyeji kwa kuupigia kura mrengo wa Kenya Kwanza.

Alitembea kote kote.

“Watu wetu, ikiwa hamungeitikia wito wetu wa kumpigia kura Rais William Ruto, sijui tungekuwa wapi. Binafsi, nilikuwa pabaya. Nilikuwa kwenye mdomo wa mnyama mkali. Angenimeza mzima mzima ikiwa hamngenichagua,” akasema Bw Gachagua.

Baada ya fungate ya kisiasa kuisha, uhalisia kamili kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa ukanda huo unaonekana kuanza kumpambazukia Bw Gachagua.

Juhudi za kujikweza kama kiongozi wa kisiasa na msemaji wa ukanda huo zinaonekana kukumbwa na changamoto.

Kiini?

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, sababu kuu ya malumbano yanayoendelea katika ukanda huo ni dhana kwamba Bw Gachagua amekosa kudumisha mshikamano wa kisiasa uliokuwepo kabla ya Bw Kenyatta kustaafu.

Kulingana na Bw Gitahi Ngunyi, ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa, “viatu alivyovaa Bw Kenyatta ni vikubwa sana kumtoshea Bw Gachagua”.

“Ukweli ni kuwa, dhana iliyopo Mlima Kenya ni kuwa haina msemaji halisi wa kisiasa. Hisia za wengi ni kwamba, eneo hili ni kama yatima kisiasa,” asema Bw Ngunyi.

Mchanganuzi huyo anasema kuwa katika miaka ya hapo nyuma, ilikuwa vigumu sana kwa viongozi katika eneo hili kulumbana, kuvutana au kulaumiana kisiasa kama ilivyo kwa sasa.

Anarejelea mchipuko wa baadhi ya wanasiasa, kama vile kiongozi wa zamani wa kundi la Mungiki, Bw Maina Njenga, kuchangiwa na dhana ya eneo hilo kuwa “yatima” kisiasa.

“Katika kujitetea kwake, Maina amekuwa akisema analenga kujaza pengo la kisiasa lililopo Mlima Kenya, kwani viongozi waliopo wameshindwa kujaza nafasi hiyo. Kauli hiyo bila shaka inaashiria kuna sehemu za ukanda huu zinazohisi kutowakilishwa kisiasa,” akaeleza mchanganuzi huyo.

Wadadisi wanasema kuwa ikiwa viongozi wa kisiasa, kidini, wazee na mabwanyenye katika eneo hilo hawatafanya kikao cha pamoja kubaini mwelekeo wake wa kisiasa, basi kuna hatari kubwa inayolikabili.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mdadisi wa masuala ya kisiasa Dkt Rita Khamisi anasema kwamba eneo liko kwenye hatari ya kujipata katika hali lililokuwa eneo la Magharibi, ambako wanasiasa wengi wamekuwa waking’ang’ania uongozi wa jamii ya Abaluhya.

“Ni lazima Bw Gachagua, Bw Kenyatta kati ya viongozi wengine kuzungumza pamoja na kubaini mwekekeo na mustakabali wa kisiasa wa eneo hilo, kabla ya hali kudorora zaidi,” akasema Dkt Khamisi ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Egerton.