Mlima Kenya njia panda katika uchaguzi wa leo Agosti 9

Mlima Kenya njia panda katika uchaguzi wa leo Agosti 9

NA MWANGI MUIRURI

UCHAGUZI mkuu unaofanyika hii leo Agosti 9 bila shaka ni tukio la kipekee kisiasa kwa wenyeji wa Mlima Kenya ambao kwa mara ya kwanza kwa miongo mingi wana fursa finyu mno ya kutoa rais mpya.

Ingawa Bw Mwaure (jina lake halisi ni Mwaura) Waihiga anayegombea kwa chama cha Agano ni mwana wao, si miongoni mwa wawaniaji wakuu.

Kinyang’anyiro hicho kinaonekana kuwa kati ya Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Hali hii ni sawa na iliyokuwapo enzi za Rais Daniel Moi kutoka 1978-2002, wakati eneo la Kati lililazimika kupigania kile ilichotamani kutoka kwa serikali.Marais Jomo Kenyatta (1963-1978), Mwai Kibaki (2002-2013) na Uhuru Kenyatta anayeondoka wote walitoka eneo hilo na kuifanya kuwa rahisi kwa eneo hilo kupata miradi ya maendeleo.

Wazee, viongozi na wenyeji wa eneo hilo wana wasiwasi kwamba eneo hilo halina umoja usiku wa kuamkia shughuli kuu ya kura.

“Wasiwasi wangu mkuu ni kwamba tunaingia kwenye chaguzi hizi tukiwa tumegawanyika. Ingekuwa bora iwapo tungechagua kambi moja ya mtu mmoja ili tunapounda serikali au upinzani, tujitose ndani tukiwa imara kama eneo ili idadi yetu iheshimiwe,” alisema msimamizi wa taaluma, Joseph Kaguthi.

Alisema tajriba yake ni kuwa serikali “hufanya kazi na idadi iliyojipanga vyema wala si makundi madogo ya watu wasio na mpangilio.”

Alisema matokeo ya kura yatazua kambi mbili za wenyeji wa Mlima Kenya wa Azimio wenyeji wa Mlima Kenya wa Kenya Kwanza ambao katika muda wa miaka mitano ijayo watakuwa wakishindania vikali mamlaka ya kisiasa.Rais Kenyatta alijadili suala hili kwa kina alipohutubia eneo hilo Jumapili jioni kupitia vituo vya redio na runinga vya lugha ya Gikuyu.

“Watu waliogawanyika hushindwa kirahisi. Watu wetu ni sharti wajue ili wafanikiwe, ni sharti waungane. Wakati wa utawala wa Moi, watu wetu walisononeka kwa sababu hawakuwa na umoja,” alisema.

“Waliokuwa mashuhuri (Mwai Kibaki na Kenneth Matiba) waliongoza kambi mbili zilizoshindania mamlaka zikiwa zimetengana. Kutokana na hayo, uchumi wetu kama Mlima Kenya ulisambaratika kwa sababu ya kugawanyika kwetu kama kabila.”

Ingawa Rais aliepuka kusema hata yeye vilevile aligawanya kura ya Mlima Kenya mnamo 2002 alipowania dhidi ya Bw Kibaki, alisema sekta muhimu kwa watu wa eneo hilo kama vile – kahawa, majanichai, maziwa, maua, pareto na pamba – zilidorora viongozi wa eneo hilo walipokuwa wakivutana.

Hofu ni kuwa mivutano hiyo hiyo ambayo imerejea kwa kishindo itanyima eneo hilo sauti ya kupigania maendeleo.

Bila kigogo wa kuwaongoza, watalazimika kushindania mamlaka katika chaguzi za siku za usoni.

Eneo hilo sasa lina kambi mbili za kisiasa zinazoshindana kudhibiti idadi.

  • Tags

You can share this post!

Makamishna na wakuu wenye kibarua uchaguzi ukifanyika

HUSSEIN HASSAN: Kenya kwenye mtihani mwingine wa kura leo

T L