Habari MsetoSiasa

Mlima Kenya tunalenga minofu 2022 – Murathe

July 7th, 2020 2 min read

KEN KIMANTHI na MWANGI MUIRURI

NAIBU Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe amekiri kuwa eneo la Mlima Kenya litanuia kupata nafasi yenye mamlaka makubwa serikalini katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika mahojiano, Bw Murathe alisema ugavi wa mamlaka katika serikali mpya itakayochukua usukani baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu lazima uzingatie wingi wa kura katika kila eneo.

Matamshi hayo yametokea wakati ambapo kuna mdahalo unaoendelea kuhusu jinsi serikali ijayo itakavyokuwa, kukiwa na matarajio ya kurekebisha katiba kuleta nafasi zaidi za uongozi upeoni ikiwemo ya Waziri Mkuu.

Kulingana na Bw Murathe, Mpango wa Maridhiano (BBI) una umuhimu mkubwa kwa hatima ya kisiasa ya Mlima Kenya.

Bw Murathe alisema kutokana na kuwa eneo la Mlima Kenya lina takriban kura milioni nane, mtu wa kutoka eneo hilo lazima apewe nafasi ambayo inalingana na idadi hiyo.

Katika siku za hivi majuzi, aliyekuwa mgombeaji urais Peter Kenneth ameibuka kama mmoja wa viongozi ambao huenda wakasimamishwa kuwakilisha Mlima Kenya katika serikali ijayo.

Bw Murathe alisema Wakenya hawafai kujihadaa kuwa Mlima Kenya haiwezi kuwa na mgombeaji mwingine wa wadhifa mkubwa baada ya Rais Kenyatta kustaafu.

“Yeye pia (Bw Kenneth) ametosha, mbona asiwe? Lakini kwanza tushughulikie ya sasa: Tukamilishe maendeleo kisha tutaona yajayo.”

Bw Kenneth alisema yuko tayari kufanya kazi na serikali ya Jubilee ili kuisaidia kuafikia maazimio yake kwa taifa.

Kando na hayo, alisema Mlima Kenya imefanikiwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura kwa hivyo wakati viongozi watakapokaa kujadiliana kuhusu ugavi wa mamlaka, eneo hilo litataka kuambiwa litapata kiasi kipi cha ‘mkate’ utakaogawanywa.

“BBI itafanyia eneo hili vyema kwa kuweka sheria thabiti za ugavi wa rasilimali kwa kuzingatia idadi ya wakazi. Kama idadi ya wakazi itatumiwa kugawa rasilimali, mwelekeo huo huo unafaa kufuatwa katika ugavi wa mamlaka ya kisiasa,” akasema.

Kiongozi huyo wa Chama cha Kenya National Congress (KNC) alifichua kwamba hivi karibuni ataandamana na Rais Kenyatta kwa ziara maeneo ya Mlima Kenya ili ajinadi kisiasa.

Mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi, alisema Mlima Kenya imejipanga kuwa na msemaji kwa hivyo wale wanaomezea mate nafasi hiyo wasubiri.

“Kwa sasa tunachotaka ni Bw Kenneth apewe nafasi katika baraza la mawaziri ili amsaidie rais wetu kuleta umoja Mlima Kenya na kujiandaa kupata nafasi katika serikali zitakazokuja miaka ijayo,” akasema Bw Ngugi.

Rais Kenyatta amekuwa akijiepusha na mijadala kuhusu atakayerithi nafasi yake ya kutoa mwelekeo wa kisiasa Mlima Kenya ifikapo mwaka wa 2022, huku kukiwa na madai kwamba amepanga kuwania nafasi ya Waziri Mkuu ikipitishwa katika BBI.

Kando na Bw Kenneth, viongozi wengine ambao wameonekana kumezea mate urithi wa kudhibiti siasa za Mlimani ni Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria, mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru, Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.