Habari Mseto

Mlima Kenya wamwomboleza John DeMathew

August 19th, 2019 1 min read

NDUNG’U GACHANE na CHARLES WASONGA

WAPENZI wa muziki wa Benga katika janibu za Mlima Kenya wanaomboleza kufuatia kifo cha mwanamuziki John Mwangi Ng’ang’a, maarufu kama John DeMathew.

Msanii huyo maarufu alifariki Jumapili jioni kwenye ajali ya barabarani karibu na mkahawa wa Blue Post katika barabara kuu ya Thika mwendo wa saa mbili za usiku.

Kamanda wa Polisi wa Thika Elenah Wamuyu alisema gari la DeMathew liligonga trela ndogo barabarani karibu na mkahawa huo maarufu.

Mwanamuziki huyo alikuwa akisafiri kutoka Mjini Thika kuelekea Murang’a na alikuwa peke yake katika gari hilo aina ya Nissan Navara Double Cabin lenye nambari ya usajili KBT 945W.

“Alikuwa akisafiri kuelekea Kenol, kaunti ya Murang’a kwenye gari lake akielekea Kenol na alipofika eneo la ajali akagonga lori la nambari ya usajili ya KCK 279F ambalo lilikuwa likiendeshwa kuelekea upande huo huo,”akasema Wamuyu.

Mbunge wa Gatanga Ngugi Nduati alisema DeMathew alikwua akitoka kuhudhuria hafla ya harambee katika klabu ya Metro Bar ya kuchanga pesa za kumsaidia mwanamuziki mwenzake Peter Kigia.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Thika Nursing Home ambako alifariki akitibiwa.

Hadi kifo chake, mwanamuziki huyo amekuwa mwenyekiti wa Shirika jipya la Akiba na Mikopo kwa jina Tamco Sacco ambalo lilibuniwa kwa lengo la kuwasaidia wanamuziki.

“Tunataka kuungana kuunda Sacco ambayo itahifadhi fedha na rasilimali zingine ndipo tukifa, familia zetu zisitegemee harambee kutupea mazishi ya heshima,” akasema mapema mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Sacco hiyo katika mkahawa wa Thika Greens, Mjini Thika.