HabariSiasa

Mlima Kenya wataka SGR ipitie kwao

May 27th, 2019 1 min read

Na GEORGE MUNENE

WAFANYABIASHARA kutoka eneo la Mlima Kenya wamelaumu serikali kuu kuwa iliwachezea shere kwa kukosa kujenga reli ya kisasa (SGR) kupitia eneo hilo.

Wafanyabiashara hao ambao ni wanachama wa Shirika la Kitaifa la Biashara, walilalamika kuwa licha ya eneo hilo kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya, serikali haikuliangazia ifaavyo wakati wa ujenzi wa reli.

“Reli ya SGR ilifaa kuanzia eneo hili kwa kuwa inachangia vikubwa kukua kwa uchumi kuliko kitu kingine chochote,” akasema John Mate, mwenyekiti wa shirika hilo tawi la Embu.

Wakizungumza mjini Sagana baada ya kumpendekeza Bi Fatma El Maawy kuwa mwaniaji wao wa kiti cha naibu mwenyekiti wa shirika hilo kitaifa, wafanyabiashara hao walitaka reli hiyo ijengwe, ama serikali ifufue reli ya zamani ambayo inatoka Nairobi hadi Nanyuki.

Reli ya SGR imejengwa kutoka Mombasa hadi Nairobi, na awamu ya pili inaendelezwa ili ifike Naivasha na baadaye kuelekea hadi kaunti za Magharibi ya nchi ambapo mpango wa awali ni kuifanya ipitie Kisumu.

Lengo kuu ni kufanya reli hiyo iunganishe Kenya na Uganda na baadaye mataifa mengine ya Afrika Mashariki ili kukuza biashara katika ukanda huu.

Bi Maawy, ambaye alikuwa mfanyakazi wa zamani katika Wizara ya Kigeni atawania kiti hicho katika uchaguzi utakaoandaliwa jijini Nairobi mnamo Juni 8.

Wafanyabiashara hao walisema wataendelea kuisukuma serikali hadi iwasikize na kuwajengea reli.

“Tunafanya kazi muhimu katika kukuza uchumi na tunafaa kuangaziwa kwa usawa. Tunalipa ushuru mwingi na hivyo tunahitaji huduma nzuri tufanye biashara bila matatizo,” akasema Bw Njogu Waweru, mwenyekiti wa shirika hilo tawi la Kirinyaga.

Wafanyabiashara hao walisema wamekuwa wakikumbana na matatizo wakati wa kusafirisha bidhaa kutokana na ukosefu wa njia bora za usafiri.

Pia walipinga kupigwa marufuku kwa bidhaa za magari zilizotumika kutoka mataifa ya nje wakisema hatua hiyo itawafanya wengi kufunga biashara.