Habari Mseto

Mlima wa nakala za ushahidi kwenye kesi ya wizi NYS

June 21st, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU anayesikiza kesi ya ufisadi dhidi ya washukiwa 41 wa sakata ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa NYS wanaoshtakiwa kwa ubadhirifu wa mamiloni ya pesa alimwamuru mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji awape washukiwa nakala za ushahidi ifikapo Juni 25, Jumatatu .

Bw Douglas Ogoti anayesikiza kesi dhidii ya  katibu mkuu wizara ya umma , jinsia na vijana Bi Lillian Wanja Muthoni Mbogo Omollo anayeshtakiwa pamoja na aliyekuwa kinara wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 39 akiwamo mwanamitindo Ann Wambere Ngirita aliagiza wapewe mabunda ya ushahidi waanze kuandaa ushahidi.

Mawakilii Cliff Ombeta alimweleza Bw Ogoti kuwa wamechoka kuomba DPP awape nakala za mashahidi. “Naomba hii korti iamuru tupewe nakala za mashahidi. Washukiwa hawa wameanza kuingiwa na woga kwamba ushujaa ninaosifika kuwa nao haupo.”

Ombi hilo liliungwa mkono na mawakili wengine 34 wakisema upande wa mashtaka umeorodhesha mashahidi 36 katika kesi moja tu na kuna kesi kumi..

“Hatuwezi kuwashauri washtakiwa na kuandaa tetezi zao. Hatujapewa nakala za ushahidi,” alisema Bw Ombeta.

Bw Ogoti aliamuru kesi hiyo itajwe tena Julai 17 2018 ndipo mawakili waeleze ikiwa walipokea nakala za usahidi kisha waeleze muda watakaochukua kuwahoji mashahidi.

Kiongozi wa mashtaka alisema amewasilisha nakala zaidi ya 100 kortini na kuwa mawakili wako huru kwenda kuzichukua kwa afisa anayechunguza kesi hiyo Inspekya Paul Waweru.

Washtakiwa walirudishwa rumande katika magereza ya Viwandani na Langata baada ya kueleza ugumu waliokumbana nao kulipa dhamana ya Sh8milioni.