Mlima wabusu Raila

Mlima wabusu Raila

Na CHARLES WASONGA

WAKAZI na viongozi wa eneo la Mlima Kenya wametoa ishara dhahiri za kumkumbatia kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kuhudhuria kwa wingi mikutano ya kisiasa katika eneo hilo huku wakiahidi kumpigia kura uchaguzini Agosti 9.

Jumamosi, walifika kwa wingi katika mkutano wa kwanza wa Azimio la Umoja mwaka huu 2022, mjini Thika ambapo waliahidi kumpigia debe hadi awe rais wa tano wa Kenya.

Tofauti na miaka ya awali walipokuwa wakivuruga mikutano yake, kabla ya Bw Odinga kuridhiana na Rais Uhuru Kenyatta kisiasa, viongozi na wananchi wa kutoka kaunti za Kiambu na Murang’a jana Jumamosi walimpokea kiongozi huyo wa ODM kwa furaha na bashasha eneo hilo.

Aliyekuwa Meya wa Thika, Bi Mumbi Ngaru alitoa kumbukumbu ya jinsi mikutano ya Bw Odinga mjini humo kuelekea chaguzi za 1997, 2007 na 2013 ilivyovurugwa na fujo kwa sababu wakazi hawakutaka siasa zake.

“Baba leo (jana Jumamosi) nimeona, nimeshuhudia mwamko mpya wa kisiasa katika mji huu wa Thika. Viongozi na wakazi wamekukumbatia kutokana na handisheki kati yako na Rais wetu Uhuru Kenyatta ambayo ilizaa Azimio la Umoja. Ni tofauti na miaka ya nyuma tuliposhambuliwa kwa mawe nilipokuleta hapa,” akasema Bi Ngaru ambaye amewahi kuhudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa ODM.

Awali, kupitia mwafaka waliowasilisha kwa Bw Odinga katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya, viongozi wa kisiasa kutoka kaunti hizo mbili walimhakikishia kuwa watamfanyia kampeni hadi aingie Ikulu mwaka huu.

“Sisi kama viongozi wa Kiambu na Murang’a na kwa niaba ya wenzetu kutoka eneo pana la Mlima Kenya tumekubaliana leo kwamba wewe Baba ndiwe tutakayeunga mkono katika uchaguzi wa urais baadaye mwaka huu. Haya ni makubaliano sio matakwa,” ukasema mwafaka huo uliosomwa na Mbunge wa Limuru, Bw Peter Mwathi.

Naye Gavana wa Kiambu, Dkt James Nyoro ambaye aliongoza ratiba ya shughuli katika mkutano huo alimpongoza Bw Odinga na Rais Kenyatta akisema handisheki yao imeleta utulivu katika kaunti hiyo na kote nchini.

“Hii ndiyo maana sisi kama viongozi na wakazi wa Kiambu na Mlima Kenya kwa jumla tunaunga mkono Azimio la Umoja ambalo lilitokana na salamu kati yako na rais wetu. Tumekubali wito wako na tutakupigia kura ili uwe rais wa tano wa taifa hili,” akasema.

Mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Thika Green ulihudhuriwa na magavana, wabunge, madiwani na mamia ya wagombeaji viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao.

Miongoni mwa magavana waliohudhuria ni mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Martin Wambora (Embu), naibu wake James Ongwae (Kisii), Francis Kimemia (Nyandarua), Lee Kinyanjui (Nakuru), Joseph Ole Lenku (Kajiado) miongoni mwa wengine kutoka nje ya Mlima Kenya.

Katika hotuba yake, Bw Odinga alikemea vikali matamshi ya uchochezi yaliyotolewa juzi na viongozi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ katika mkutano wa kisiasa uliofanyika mjini Eldoret.

Alisema serikali yake itaupa usalama wa Wakenya kipaumbele wala haitaruhusu ghasia za kisiasa na za kikabila zilizoshuhudiwa wakati wa chaguzi za 1992, 1997, 2007 na 2013.

Bw Odinga alikariri kuwa Wakenya wako huru kuishi na kufanya kazi katika sehemu yoyote nchini bila kutishwa.

“Hii ndiyo maana hatutaki kusikia matamshi kama vile “madoadoa” na “kwekwe” kwa sababu yanaibua kumbukumbu ya ghasia zilizoshuhudia kabla na baada ya chaguzi zilizopita,” akaeleza.

Akaongeza: “Mkikuyu anaweza kuishi Homa Bay, Eldoret au popote nchini, sawa na Mjaluo au Mluhya. Hii ni kwa sababu sote tu Wakenya. Kwa hivyo, tunawalaani wale ambao wiki jana waliwaita Wakenya wengine ‘madoadoa’ au kumwambia kiongozi fulani wa asili ya Kihindi kule Eldoret kwamba arudi Punjab. Hii nchi ni yetu sote.”

Alitetea mpango wake wa kutoa Sh6,000 kila mwezi kwa familia masikini akisema utaweza kuutekeleza “kwa sababu nimewahi kuwa Waziri Mkuu na ninaelewa mahala ambapo pesa zipo.”

  • Tags

You can share this post!

Kauli za ‘wafia Ruto’ zinavyopunguza ufuasi wake Mlimani

Naunga Raila kwa sasa ila macho yangu yako kwa urais 2027...

T L