Mlipuko usiku waibua hofu kijijini Lamu

Mlipuko usiku waibua hofu kijijini Lamu

Na KALUME KAZUNGU

TAHARUKI imetanda katika kijiji cha Kiunga kilicho mpakani mwa Lamu na Somalia, baada ya mlipuko mkubwa kutokea usiku wa manane katika nyumba ya mwanamume aliyepotea katika hali tatanishi.

Baadhi ya wakazi walidai mlipuko huo katika nyumba ya Yasir Mahmoud Ahmed – ambaye alitoweka miezi sita iliyopita – ulisababishwa na bomu lililorushwa kutoka angani.

Familia yake na wakazi wa hapo wameelezea hofu yao kuhusiana na mkasa huo, na baadhi waliamua kuhamia maeneo mengine ya Lamu kwa kuhofia kulengwa kimakosa.

Mji wa Kiunga uko ndani ya eneo la operesheni inayoendelea ya kufurusha magaidi na kuweka amani msituni Boni.

Bw Mahmoud Ahmed Abdulkadir, ambaye ni babake Yasir, alisema inatia hofu ikiwa sasa mabomu yanayorushwa kutoka angani yataanza kutumiwa katika oparesheni za kiusalama ndani ya nchi.

“Nilipigiwa simu na mke wa Yasir majira ya saa nane alfajiri Jumanne, kuaniarifu kuwa nyumba ya mwanangu ilikuwa imepigwa bomu. Naambiwa kuna ndege ilipita kabla ya mlipuko kusikika. Ningeomba serikali kuihakikishia familia ya mwanangu usalama. Tukio hili limetutia hofu,” alieleza Bw Abdulkadir.

Bw Mahmoud Ahmed Abdulkadir maarufu kama Ustadh Mau ndiye baba mzazi wa Yasir Mahmoud Ahmed anasema familia yake inafuatiliwa baada ya tukio la Novemba 30, 2021, ambapo duka na mali ya mwanawe iliharibiwa kwa moto. PICHA | KALUME KAZUNGU

Chanzo halisi cha mlipuko huo hakikubainika mara moja, huku serikali ikijitenga na lawama za wanakijiji.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia, aliambia Taifa Leo kuwa walinda usalama wa nchi hawakuhusika katika kisa hicho.

Kulingana naye, kuna uwezekano moto ulisababishwa na mitungi ya gesi iliyokuwa ndani ya jengo hilo.

“Nilifahamishwa kuwa duka lilikuwa na mitungi ya gesi ambayo ililipuka na kuchoma nyumba. Maafisa wetu walisaidia kuuzima moto. Hawajachangia kivyovyote mkasa huo. Kazi yetu kama serikali ni kulinda wananchi na mali,” akasema Bw Macharia.

Mnamo Juni 19, 2021, Yasir, 43, alikamatwa na watu waliojihami kwa bunduki ambao wanaaminika kuwa maafisa wa usalama, katika eneo la Mkunumbi kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Ni mmoja wa wanaume wengi Pwani ambao hutoweka kwa njia zisizoeleweka, wengi wao wakidaiwa kuwa washukiwa wa ugaidi.

Kufikia sasa, familia yake haijafahamu aliko.

Afisa wa shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa, Bw Hussein Khalid, aliiomba idara ya usalama kufanya kikao na wakazi wa Kiunga ili kuwajulisha kinachoendelea.

“Lazima suala lolote – iwe ni operesheni ya usalama inaendelea mahali ama nini – watu wajulishwe ili kuondoa wasiwasi. Wakuu wa usalama Lamu waandae kikao cha dharura na wananchi wa Kiunga. Wawe tayari kujibu dukuduku zao zote,” akaeleza Bw Khalid.

Bw Ahmed Walid ambaye ni binamu ya Yasir, aliitaka serikali itende haki kwa familia yake.Wazee wa Nyumba Kumi waliozungumza na Taifa Leo walikiri kuwa baadhi ya wakazi wameanza kuhama nyumba zao.

Operesheni ya usalama katika msitu wa Boni ilizinduliwa na serikali Septemba 2015.

Lengo lilikuwa kuwasaka na kuwamaliza magaidi wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo pana.

You can share this post!

Wasiwasi migawanyiko itamponza Raila, ODM

TAHARIRI: Ya Mwendwa yameisha, tuboreshe soka sasa

T L