Kimataifa

Milipuko ya mabomu Iran yaua 103 katika makumbusho ya Qasem Soleimani

January 3rd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

TAFSIRI: FATUMA BARIKI

TEHRAN, IRAN

Milipuko miwili ya mabomu imeua takriban waombolezaji 103 Jumatano Januari 3, 2024 wakati wa mkumbusho ya aliyekuwa jenerali Qasem Soleimani aliyeuawa na kombora la Amerika miaka minne iliyopita.

Taarifa zinasema kwamba milipuko hiyo — ambayo kufikia wakati wa kupeperusha habari haikuwa imetambuliwa mhusika mkuu – ilijiri wakati ambapo kuna taharuki kubwa Mashariki ya Kati kufuatia mapigano yanayoendelea kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza haswa mauaji ya kiongozi wa ngazi za juu wa Hamas, nchini Lebanon, Jumanne.

Milipuko hiyo, ambayo iliachana kwa dakika 15, ilitokea katika Makaburi ya Wafiadini, katika msikiti wa Saheb al-Zaman, mjini Kerman ambapo ndio eneo la kuzaliwa la Soleimani, wakati wafuasi wake walipokongamana kwa makumbusho ya miaka minne tangu alipouawa na kombora la droni lililorushwa na Amerika 2020 jijini Baghdad, Iraq.

“Idadi ya watu waliouawa ilipanda hadi 103 baada ya majeruhi wa awali kufariki kufuatia mkasa huo,” shirika la habari la IRNA likasema huku runinga ya kitaifa ikisema watu 211 wamejeruhiwa, wengine wakiwa katika hali mahututi.

Baadhi ya waliouawa ni wahudumu wa afya waliokimbilia eneo hilo kuokoa majeruhi baada ya mlipuko wa kwanza.

Rais Ebrahim Raisi amekemea vikali uvamizi huo huku taifa hilo la Kiislamu likitangaza Alhamisi kuwa siku ya kitaifa ya maombolezo.

Shirikal la habari la Tasnim likinukuu kile walichosema ni chanzo cha kuaminika cha habari, lilisema kwamba mifuko miwili iliyokuwa imebeba mabomu ililipuka na kwamba washambuliaji walitekeleza ulipuaji huo kwa kutumia rimoti.

Video zilizotundikwa mitandaoni zinaonyesha halaiki ya watu walioingiwa na hofu kubwa wakitafuta kwa kutorokea huku maafisa wa usalama wakijaribu kukabiliana na hali hiyo ya dharura.

Runinga ya kitaifa nchini humo ilionyesha waathiriwa waliolowa damu wakilala chini huku ambulansi na waokoaji wakikazana kuwashughulikia.

“Tulikuwa tunatembea kwenda kwenye makaburi wakati gari lilisimama ghafla nyuma yetu na mfuko wa takataka uliokuwa na bomu kulipuka,” mmoja wa walioshuhudia alinukuliwa akisema.

“Tulisikia tu mlipuko na tukaona watu wakianguka.”

Kufikia usiku, makundi yalirudi kwenye eneo hilo la makaburi yakiimba: “Israel ife” na “Amerika ife”.

Soleimani, ambaye miaka kadhaa iliyopita alikuwa ametajwa kama “mfiadini aliyehai” alikuwa anatambuliwa kama shujaa wa Iran kutokana na mchango wake katika kuangamiza IS nchini Iraq na Syria.

Hata hivyo, taifa la Amerika na washirika wake kwa miaka mingi walimchukuliwa kuwa adui.