Dondoo

Mlo wa bei ghali wafanya kidosho ajipate singo

May 24th, 2018 1 min read

Na LEAH MAKENA

KARIOBANGI, NAIROBI

KIDOSHO mmoja mtaani hapa aliachwa mataani baada ya kushindwa kudhibiti tamaa yake ya kupenda samaki kila alipokutana na mpenzi wake.

Habari zasema kuwa kidosho alizoea kumtaka jamaa kumnunulia samaki kila alipozuru kwake au walipopata nafasi ya kula mikahawani, tabia iliyokuwa ikimuudhi jamaa.

Siku chache za kwanza, jamaa alifika kwa kidosho akiwa na samaki ila akashangaa mwanadada alipoanza kumlazimisha kufika kwake na samaki bila kujali iwapo alikuwa na pesa au la.

Juhudi za jamaa kujitetea ziliambulia patupu kwani kidosho alisisitiza kuwa ulikuwa wajibu wake kumlisha kwa kila alichotaka na kushughulikia mahitaji yake kama ishara ya kuonyesha angemtunza akimuoa.

Siku ya kioja, jamaa alimvutia kidosho waya na kumtaka wakutane kwenye hoteli moja mjini ili wazungumze na hapo ndipo mambo yalitumbukia nyongo.

Mwanadada alitonesha kidonda alipomtaka weita kumletea samaki licha ya jamaa kuitisha vinywaji kwa kuwa mazungumzo yalipangiwa kuchukua muda mfupi.

Hapo ndipo jamaa alipandwa na mori na kuanza kumkemea mwanadada kwa kutaka kutumia pesa zake kiholela.

“Unadhani huwa ninaokota pesa barabarani? Haunipendi ila ni pesa zangu unataka kufuja. Hiyo sahani ya ugali na samaki uliyoitisha utalipa wewe ili ujue ninayopitia,” jamaa alisema na kusimama.

Inasemekana kuwa polo alimuonyesha kidosho mgongo baada ya kulipia chupa mbili za soda alizokuwa ameitisha na kumtaka mwanadada kuzibugia zote.

Duru zasema kuwa mrembo alilazimika kulipa deni huku akijuta kutofuata agizo la jamaa.

Huo ndio ulikuwa mwisho wa uhusiano huo kwani kidosho hakufanikiwa kumpata jamaa tena.

…WAZO BONZO…