Habari

MLUNGULA: Mkurugenzi mkuu wa Kebs akamatwa

July 2nd, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na MARY WANGARI

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Ukadiriaji Ubora wa Bidhaa (Kebs) Benard Njiraini alikamatwa Alhamisi asubuhi kwa tuhuma za ufisadi.

Njiraini alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) nyumbani kwake na kupelekwa katika makao makuu ya tume hiyo jumba la Integrity, Nairobi kuhojiwa.

Anakabiliwa na tuhuma za kushirikiana na maafisa wa upelelezi ambao wamekuwa wakichungu sakata ya ukiukaji wa sheria za ununuzi katika utoaji wa zabuni kwa kampuni za kukagua ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini.

“Leo (Alhamisi) maafisa wa EACC wamemkamata Bw Benard Njiraini kuwa kosa la kutotii maagizo aliyopewa kuhusiana na sheria ya kupambana na ufisadi ya 2003. Alifeli kupeana stakabadhi muhimu zilizohitajika kuwezesha kukamilisha kwa uchunguzi kuhusu sakata ya ufisadi katika shirika hilo,” EACC ikasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

EACC imekuwa ikichunguza madai kwamba maafisa wa Kebs walipokea hongo ili kupeana zabuni ya ukaguzi wa bidhaa kama magari ya mitumba na bidhaa za kieletroniki, vipuri na bidhaa nyinginezo ambazo huingizwa nchini kutoka ng’ambo.

Amekamatwa na makachero halafu akapelekwa katika makao makuu ya EACC katika jengo la Integrity Center, Nairobi, ambapo aliandikisha taarifa.

Kulingana na taarifa kutoka kwa shirika hilo la kupambana na ufisadi, Njiraini alikamatwa kwa kile kilichotajwa kama kutatiza uchunguzi hivyo kulemaza juhudi za EACC katika mchakato huo.

EACC imemkamata Bw Benard Njiraini kama hatua ya kisheria kwa kukosa kutii notisi aliyopatiwa kuambatana na Kipengele 27 na Kipengele 66 cha Sheria kuhusu Kupambana na Ufisadi na Hatia za Kiuchumi Nambari 3 ya 2003.

“Hii ni kwa nia ya kupata stakabadhi hizo na kuwasilisha mashtaka dhidi yake kwa ukiukaji wake,” kimesema kijisehemu cha taarifa hiyo.

Pia anatuhumiwa kutatiza juhudi za kufanyia uchunguzi vitendo vya ufisadi katika mchakato wa utowaji zabuni kwa motokaa kuukuu, vifaa vya rununu na vipuri vyake pamoja na kanuni za uuzaji bidhaa katika mataifa ya kigeni.

Hatua hiyo imejiri hata kabla yam waka mmoja kuisha tangu Njiraini alipoteuliwa kama mkurugenzi wa Kebs mnamo Agosti 2019 ambapo aliahidi kuangamiza ufisadi uliokithiri katika halmashauri hiyo ya kitaifa.

Njiraini alichukua usukani kutoka kwa Charles Ongwae aliyekuwa mkurugenzi wa Kebs na ambaye alirushwa nje mnamo Januari 2019 kuhusiana na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kutowasilisha kodi kwa serikali.