Habari za Kitaifa

Mmiliki wa kiwanda cha gesi ya janga aachiliwa kwa dhamana

February 28th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MMILIKI wa kiwanda cha gesi iliyolipuka na kusababisha maafa Embakasi ameachiliwa kwa dhamana huku maafisa wa Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira Nchini (Nema) wakiachiliwa huru na Mahakama Kuu.

Mkasa huo wa gesi kulipuka ulisababisha vifo vya watu 12 huku wengine 600 wakiachwa na majeraha.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Dolphina Alego alimwachilia Derick Kimathi kwa dhamana ya Sh2 milioni baada ya kukataa ombi la polisi waliotaka waruhusiwe kumzuilia kwa siku 14 zaidi.

Katika uamuzi wake, Bi Alego alisema polisi wamemzuilia mshukiwa huyo kwa siku 21.

Alisema kuendelea kumzuilia mshukiwa huyu kwa siku nyingine 14 huku polisi wakiendelea na uchunguzi itakuwa ni ukiukaji wa haki zake.

Akiomba akubaliwe kumzuilia Bw Kimathi kwa siku 14 zaidi, Inspekta Isaac Kariuki alisema uchunguzi unaendelea na kwamba wameandikisha taarifa kutoka kwa majeruhi 300.

Pia alisema wanatarajia kuandikisha taarifa za watu wengine 30.

Bw Kariuki alimweleza hakimu kwamba polisi wanatazamia kufika Tanzania na Uganda ambapo gesi iliyosababisha maafa eneo la Embakasi ilikuwa imetolewa na kupelekwa mtawalia.

Bw Kimathi na maafisa watatu wa Nema walikuwa wamezuiliwa kwa siku 21 katika kituo cha polisi cha Embakasi.

Bw Kimathi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Maxxis Energy Nairobi Limited pamoja na maafisa wa Nema Bw Joseph Makau, Bi Marrian Mutete Kioko na Bw David Warunya On’gare waliachiliwa kwa dhamana japo wakaonywa wasivuruge uchunguzi.

Bi Alego aliamuru Bw Kimathi, Bw Makau na Bi Kioko walipofikishwa kortini wazuiliwe katika kituo cha Polisi cha Embakasi naye Bw Ong’are azuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill ili awe karibu na hospitali kwa vile alikuwa akiugua.

Hakimu alisema mshukiwa huyo “alihitaji kuwa karibu na hospitali kutokana na hali yake ya kiafya.”

Mawakili Odero Okello na Karathe Wandugi wanaowatetea washukiwa hao, walieleza mahakama Bw Ong’are alihitaji huduma za matibabu na hakufaa kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi.

Hakimu alikuwa ameombwa aagize mshukiwa huyo apelekwe katika Hospitali ya Karen kupokea matibabu huku polisi wakiendelea na uchunguzi wao.

Akikubali ombi la viongozi wa mashtaka Herbat Isonye, Dorcus Rugut, Sonia Njoki, na James Gachoka kwamba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 21, hakimu alisema polisi walihitaji muda kuchunguza kesi hiyo kwa kina.