Habari Mseto

Mmoja auawa na majambazi kwenye baa

November 17th, 2020 1 min read

GEORGE MUNENE NA FAUSTINE NGILA

Mwanamume mmoja alidungwa kisu hadi akafariki na mwingine akapata majeraha nje ya baa moja mjini Runyenjes Kaunti ya Embu.

Aliyepata majeraha anapigania uhai wake kwenye hospitali ya Kaunti ndogo ya Runyejes ambapo alikimbizwa baada ya tukio hilo lililozua hofu eneo hilo.

Kulingana na habari za wakazi mwanamume huyo aliyefariki wa miaka 21 Victor Murithi Mwiti alikuwa amesimama nje ya baa hilo akiwa na mwenzake walipovamiwa na wavamizi.

Bila ya uchochezi wavamizi hao walitoa kisu kutoka mfukoni na wakawavamia wawili hao huku wakimuua Bw Mwiti. Wavamizi hao walikimbia wakajificha.

Baadaye polisi waliwasili kwenye eneo la tukio na wakabeba mwili wa Bw Mwiti huku mwezake akipelekwa hospitali.

Baadaye wapelezi waliwakamata washukiwa walipokuwa wamejificha na wakawafungia kwenye kituo cha polisi ili wahojiwe.

Mkuu wa polisi wa Runyenjes Benjamin Muhia alisema kwamba wanafanya uchunguzi ili kubaini  sababu ya mavamizi hayo.

“Tumekamata mvamizi huyo na anaweza shtakiwa kwa mauaji na uvamizi baada ya kumaliza uchunguzi,”alisema Bw Muhia.

Wakazi walisema kwamba walishuku kwamba mvamizi huyo alikuwa ametumia dawa za kulevya  wakati alitekeleza kitendo hicho cha uhalifu.