MMvita Youngstars yailima Annex 07 FC 3-0

MMvita Youngstars yailima Annex 07 FC 3-0

NA CHARLES ONGADI,

MOMBASA

MVITA Youngstars FC iliendeleza msururu wa matokeo mazuri katika Ligi ya Mombasa Primia inayoandaliwa na Chama cha Soka kaunti ya Mombasa (MCFA).

Mvita Youngstars inayofunzwa na Fahad Abdulaziz, iliipepeta Annex 07 FC mabao 3-0 katika pambano lililogaragazwa uwanjani Shimo la Tewa Annex, Kisauni.

Timu zote zilikuwa nguvu sawa bila kufungana bao lolote katika kipindi cha kwanza cha mchezo lakini wachezaji wa Mvita Youngstars wakaanza kipindi cha pili kwa kasi ya ajabu.

Maxwel Ng’ang’a alicheka na nyavu mara mbili katika dakika ya 55 na 67 kisha Abdulmajid Ahmed akadungilia msumari wa mwisho kunako dakika ya 78.

Hata hivyo, akizunguza na Taifa Leo Digitali baada ya pambano hili, kocha mkuu wa Annex 07 Nathaniel Malau alisema kikosi chake kilishindwa kutamba kutokana na baadhi ya wachezaji wake tegemeo kujeruhiwa katika pambano lao la awali.

“ Tumecheza mechi hii bila straika na ngome yetu ilivuja sana kutokana na kukosekana kwa nyota wetu Patrick Wanje aliyejeruhiwa katika mechi yetu dhidi ya Nyali Youth,” akalalama kocha Malau.

Lakini mwezake wa Mvita Youngstars Fahad Abdulaziz alisema walijiandaa vyema wa mechi hii hasa ikitiliwa maanani kwamba wapinzani wao waliwahi kuwashinda msimu uliopita kwa mabao 3-2.

Kocha Fahad : “ Tumecheza kama sisi na kvuna ushindi huu ambao ni sawa na kulipiza kisasi kwa matokeo ya msimu uliopita.”

Katika matokeo mengine ya Ligi hii yaliyochezwa wikendi hii, Bamburi United FC ilitoka sare 2-2 na Westham katika mchuano uliochezwa uwanjani Parmasharp, Bamburi.

Gurdforce FC naGolden Boys zikaumiza nyasi bia lkufungana katika pambano lililoandaliwa uwanjani Peleleza, Likoni huku Soweto ikiiliza Zaragoza 2-0.

Junda Strikers ikaikung’uta Mantubilla 3-0 nayo Mikindani Youngstars ikiibamiza Tononoka Sports 5-2, Bandari Youth ikaikung’uta Coolchester 2-0.

Katika matokeo ya mechi ya Daraja la Kwanza, Goodhope FC na Majaoni City ziliagana sare ya 2-2 wakati Cosmos na Peru zikifungana 1-1.

Likoni Combined ikailaza High Level 2-0, Bantu Warriors ikailiza Bilima Youth 2-0 nayo Daytona ikaikunja Jomvu Youngstars 2-1.

Katika Ligi ya Wazee (Mombasa Veterans League), Wazee Health iliicharaza Coolchester 5-1 nayo Mikadini Veterans ikazima Fetuwe 2-0.

You can share this post!

Soko ya Daraja la Pili yapamba moto Pwani

Maneja wa Bandari asifu kikosi chake kwa kuzima Ulinzi