Habari

Mnada: Wengi wafika kituo cha polisi Thika kununua magari na pikipiki

July 5th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MNADA wa kuuza magari na pikipiki ambazo zimeegeshwa kwa muda mrefu katika kituo cha Polisi cha Thika umefanyika Ijumaa mbele ya wakazi wengi.

Kampuni ya Wiskam Auctioneers ndiyo ilipewa jukumu la kuendesha shughuli hiyo ambapo magari 47 na pikipiki 120 zinatarajiwa kuuziwa watakaomudu.

Naibu mkuu wa Polisi wa Thika Magharibi, Bw Benard Ayoo, amesema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya magari yaliyopata ajali pamoja na pikipiki kujaza eneo la kituo hicho.

“Baada ya kupata mwelekeo kutoka kwa mahakama tulitangaza rasmi kwa vyombo vya habari kuhusu uuzaji wa magari hayo kwa kupigwa mnanda. Kila mmoja ana ruhusa kuja kujichagulia gari ama pikipiki itakayomfaa,” alisema Bw Ayoo.

Alisema magari yatauzwa kuanzia bei ya Sh 50,000 nazo pikipiki ni kuanzia Sh 10,000 kama tangazo la mwanzo.

Amesema hatua hiyo itakuwa muhimu kwa sababu hata mazingira ya kituo cha Polisi yatakuwa sawa.

Ameongeza kuwa magari mengi yameegeshwa kituoni hapo kwa zaidi ya miezi sita, muda anaosema ni muda mrefu zaidi.

Mfanyakazi wa Wiskam Auctioneer, Bw Mureithi Kariuki amesema lengo lao kuu lilikuwa kuona ya kwamba wanafanikisha shughuli hiyo pamoja na kuhakikisha ya kwamba waliofika kununua magari hayo na pikipiki wanatendewa haki bila kubaguliwa.

“Lengo letu ni kuona ya kwamba yeyote anayefika kiwango cha juu zaidi kuliko wengine ndiye anapewa nafasi ya kununua. Baadaye serikali itafanya juhudi kuona ya kwamba stakabadhi zote muhimu zinapatikana bila shida,” amehakikisha Bw Kariuki.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwa wingi kukagua magari na pikipiki zilizopigwa mnada Julai 5, 2019, mjini Thika. Picha/ Lawrence Ongaro

Bw David Githoga ambaye ni muuzaji wa magazeti ya Daily Nation na Taifa Leo, amesema anataka kujitafutia pikipiki ambayo itamsaidia kusafiri maeneo tofauti akiuza magazeti.

“Nimetembea kwa miguu muda mrefu na kwa hivyo leo nitafanya juhudi kuona ya kwamba ninanunua pikipiki kwa bei nafuu,” amesema Bw Githoga.

Baadhi ya pikipiki katika kituo cha Polisi cha Thika zikipigwa mnada. Picha/ Lawrence Ongaro

Naye Ephantus Mwangi amesema anataka kununua gari dogo ambalo litamsaidia kusafiri hadi maeneo mbalimbali.

“Hata hivyo baada ya kununua gari hapa ni sharti uwe na pesa kiasi fulazi za kulifanyia marekebisho ya hapa na pale. Kwa hivyo pia watu wale wanaokimbilia magari hayo ni lazima wawe na fedha zingine za ziada ili kufanikisha mipango yote awaliokuwa nayo,” amesema Bw Mwangi.

Hata hivyo, wanabodaboda wengi waliodhani kuwa pikipiki hizo zingeuzwa kwa bei ya chini kabisa kuliko kiwango kilichotajwa cha chini walirejea makwao wakiwa wamevunjika moyo kwani wengi wao walikuwa na pesa chache mfukoni.