Habari Mseto

Mnadhimu mpya wa Jubilee katika seneti atetea mabadiliko ya uongozi yaliyofanywa

May 12th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

SENETA wa Murang’a Irungu Kang’ata ametetea mabadiliko ya uongozi wa bunge la seneti katika chama tawala cha Jubilee (JP).

Kwenye mabadiliko yaliyofanywa Jumatatu katika Ikulu ya Rais, Nairobi, kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen (JP) aliondolewa madarakani na nafasi yake kuchukuliwa na seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio (Kanu).

Vilevile, nafasi ya kiranja wa seneti iliyoshikiliwa na Seneta wa Nakuru Susan Kihika ambaye pia ni mwanachama wa JP, ilikabidhiwa seneta Kang’ata.

Ni mabadiliko yaliyokosolewa na kupokea upinzani mkali, yakionekana kulenga viongozi wa mrengo wa ‘Tangatanga’ unaoegemea upande wa Naibu wa Rais William Ruto na ambao umekuwa ukirushiana cheche za maneno na ule wa ‘Kieleweke’ unaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

Viongozi walioathirika na ambao ni wandani wa Dkt Ruto, wanashikilia wangali mamlakani, wakihoji “sheria za chama hazikufuatwa kufanya uteuzi huo haramu”.

Mkutano huo wa Ikulu na ambao Naibu wa Rais hakuuhudhuria, ulihudhuriwa na maseneta ‘waalikwa’ wanaomuunga mkono Rais Kenyatta.

Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata Jumanne amesema mageuzi hayo ni ya kawaida katika mabaliko ya chama chochote kile.

“Hayo ni mabadiliko ya kawaida katika chama chochote kile. Pia tumeona chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kikifanya mabadiliko yake. Leo wewe ni kiranja, kesho haupo katika wadhifa huo. Leo wewe ni kiongozi wa wengi bungeni, kesho haupo katika wadhifa huo,” seneta huyo akasema.

Seneta Murkomen na Kihika, wamedai kwamba ni maseneta wachache mno waliohudhuria mkutano huo wa faragha Ikulu, wakieleza kwamba 22 hawakupata mwaliko.

Hata hivyo, Bw Kang’ata anasema waliokosa kuhudhuria ilikuwa kwa hiari yao.

“Baadhi ya maseneta waliamua kutohudhuria kwa hiari,” akasema.

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanahoji mabadiliko yanayoshuhudiwa katika chama tawala cha Jubilee, ni njia mojawapo kulemaza juhudi za Naibu Rais Ruto kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Tangu salamu za maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 2018, maarufu kama handisheki, uhusiano wa Rais na naibu wake umeonekana kusambaratika, ahadi ya Rais Kenyatta kumuunga mkono Dkt Ruto 2022 kuwania urais ikichukua mkondo tofauti.