Habari za Kitaifa

Mnatunyima bomba la mafuta kwa nini? Uganda yashtaki Kenya EACJ

January 3rd, 2024 2 min read

Na SAM KIPLAGAT

UGANDA imeishtaki Kenya kwa kuiwekea vikwazo kampuni yake ya mafuta kutumia mabomba ya Kampuni ya Usafirishaji Mafuta nchini (KPC) kusafirisha bidhaa zake za petroli kutoka bandari ya Mombasa.

Haya yanajiri wiki chache baada ya Rais William Ruto kukanusha kuwepo kwa tofauti zozote kati yake na mwenzake wa Uganda, Bw Yoweri Museveni kuhusu masuala ya usafirishaji wa mafuta.

Katika kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Mwanasheria Mkuu wa Uganda anaishutumu Kenya kwa kukiuka vipengele kadhaa vinavyounda Muafaka wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na utaratibu wa kuanzishwa kwa Soko la Pamoja la Jumuiya hiyo (EACCM).

Uganda inasema kwenye kesi yake katika mahakama ya EACJ kwamba haihitaji leseni kutoka kwa Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta nchini (EPRA) kutumia mabomba ya KPC kusafirisha bidhaa zake za petroli.

Taifa hilo jirani linataka mahakama hiyo kuamua kwamba vikwazo vilivyowekwa na mamlaka ya EPRA na agizo kutoka Mahakama Kuu ya Kenya, Desemba mwaka jana, ikizuia mamlaka hiyo kuipa UNOC leseni, vinakiuka vipengele vilivyobuni Muafaka wa EAC.

“Mahakama ya EACJ inafaa kuagiza Kenya itoe kibali kwa UNOC, kwa masharti ya kibiashara, itumie mabomba ya KPC kama mtoaji huduma hiyo kwa mataifa mengine wanachama au asasi yoyote ile,” zinasema stakabadhi za kesi hiyo.

Uganda huagiza asilimia 90 ya mafuta yake, yaliyosafishwa, kupitia Bandari ya Mombasa na kisha kusafirishwa na KPC.

Kwa muda mrefu, bidhaa hizo hushughulikiwa na Kampuni za Kuuza Mafuta, zinazohudumu Kenya, na zilizopewa zabuni chini ya makubaliano kati ya serikali za Kenya na Uganda.

Kisha kampuni hizo huuza bidhaa hizo kwa kampuni za kuendesha biashara ya uuzaji mafuta (OMCs) nchini Uganda.

Uganda, nchi isiyo na bandari, inasema mtindo huu wa kutegemea kampuni za Kenya (OMCs) kuagiza na kuiuzia bidhaa za petroli umeiweka katika hali hatari ambayo imechangia kupanda kwa bei ya rejereja ya bidhaa hizo.

Mwaka jana, Uganda ilibadili sera yake kuhusu ununuzi, uagizaji na usambazaji mafuta kwa kutwika kampuni ya UNOC majukumu hayo yote.

Hii ina maana kuwa kampuni hiyo inayomilikiwa na serikali ya Uganda ndio ya kipekee ya kuagiza na kusambaza bidhaa zote za petroli kwa masoko yake.

Baadaye kampuni ya UNOC ilianzisha mazungumzo na Kenya kuhusu mabadiliko hayo na inadaiwa Kenya iliahidi kushirikiana na taifa hilo jirani katika kufanikisha utekelezaji wa sera hiyo mpya.

Ili kutekeleza mpango huo, UNOC inasema iliomba kukubaliana na KPC kuhusu uhifadhi na usafirishaji wa mafuta yake.

Baadaye kampuni hiyo ya Uganda ilihitajika kufikia mahitaji mengine ya kisheria kutoka kwa EPRA, kama vile leseni za uagizaji na uuza bidhaa za mafuta (sio gesi).

Leseni hiyo ingeiruhusu Uganda kutumia miundo msingi ya KPC kusafirisha mafuta yake kutoka Bandari ya Mombasa hadi Kampala.

Mwanasheria Mkuu wa Uganda anasema chini ya kanuni ya EPRA, taifa hilo lilihitajika kuanzisha kampuni nyingine au UNOC isajiliwe au ianzishe tawi jipya nchini Kenya.

Lakini Uganda inasema masharti hayo hayana maana mbali na kuwa kikwazo kwa utekelezaji wa mpango wake mpya.

Hata hivyo, ilianzisha tawi la UNOC nchini Kenya lenye jukumu la kutayarisha leseni.

Stakabadhi zilizowasilishwa na Uganda katika mahakama ya EACJ zinasema kuwa UNOC ilihitajika kuwasilisha stakabadhi nyingi na kutimiza mahitaji kadhaa kuiwezesha kupewa leseni hiyo.

Mahitaji hayo yanajumuisha cheti cha usajili wa kampuni kutoka kwa Msajili wa Kampuni, nakala za vitambulisho vya kitaifa au paspoti za wakurugenzi wote, vyeti vya kufanya kazi vya wakurugenzi wote watakaofanya nchini Kenya na cheti cha ulipaji ushuru kutoka Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA).