Habari Mseto

Mnayedai nilimdhulumu kimapenzi ni mke wangu – Mshtakiwa

February 20th, 2019 1 min read

Na CHARLES WANYORO

MWANAMUME Jumatano alishangaza mahakama ya Meru baada ya kudai kwamba msichana wa miaka 17 ambaye ameshtakiwa kwa kumdhulumu kimapenzi ni mkewe.

Rodgers Kariuki alimwambia Hakimu Mkazi wa Meru, Edward Tsimonjero kwamba mahakama inapaswa kumwachilia kwani amekuwa akiishi na msichana huyo kama mkewe kwa miaka saba kumaanisha alimuoa akiwa wa miaka 10.

Alishtakiwa kumdhulumu kimapenzi mlalamishi kati ya 2014 na Machi 29, 2018 katika eneo la Gitimbine, Kaunti ya Meru.

Hata hivyo, mshukiwa, aliye na zaidi yaa miaka 30, alimshangaza hakimu kwa kumwambia kwamba mlalamishi ni mkewe.

Baadaye alikiri shtaka jingine la kumgusa mlalamishi sehemu zake za siri hali iliyomfanya hakimu kumuuliza ikiwa alifahamu uzito wa mashtaka yaliyomkabili.

Kiongozi wa Mashtaka, James Kinyua aliiambia mahakama kwamba mshukiwa amekuwa akikwepa kufika mahakamani baada ya kushtakiwa mara ya kwanza mnamo 2015. Alikamatwa baada ya polisi kupashwa alikokuwa.

Bw Kinyua aliiomba mahakama kuondoa dhamana aliyopewa na kumzuilia katika rumande.

Hakimu alisema kwamba dai lake kwamba mlalamishi ni mkewe lilimpa haki ya kujitetea dhidi ya mashtaka hayo. Alisema ikizingatiwa mshtakiwa alikuwa amekwepa kufika kortini awali azuiliwe rumande.