Habari Mseto

Mng'oa meno aamriwa asikizane na shemeji zake

March 6th, 2018 2 min read

Kutoka kushoto: Ashman Sapra, Dkt Nisha Sapra na Bi Kuldip Sapra wakiwa katika Mahakama ya Milimani Machi 5, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

DAKTARI wa kung’oa meno na shemeji zake wawili Jumatatu walipewa muda wa wiki moja waafikiane kuhusu ugavi wa mali ya Sh700 milioni wanayong’ang’ania.

Hata hivyo Dkt Nisha Sapra  alielezea waziwazi kwamba shemeji wake wawili Kuldip Sapra na Ashman Madan Sapra “ hawatamsikiza kwa vile wanasema alimuua ndugu yao Yogesh Sapra  miaka 13 iliyopita.”

Pia Dkt Sapra alimweleza hakimu mkuu  Bw Francis Andayi kwamba hajui kama haki itatendeka kabla ya kuamuliwa kwa kesi inayomkabili ya kumuua mumewe Yogesh Agosti 2005.

Lakini Bw Andayi aliwaeleza watatu hao Kuldip , Ashman na Dkt Sapra kwamba “kesi zote zilizo katika Mahakama za Kenya kuhusu mali ya Yogesh zitafikia tamati siku moja hata kama zitachukua miaka mingapi.”

Bw Andayi aliyekuwa anatarajiwa kusoma uamuzi iwapo Kuldip na Ashman wataagizwa wajibu mashtaka manne ya ugushi wa stakabadhi kuhusu ugavi wa mali aliyoacha Yogesh alipoaga ilichukua mkondo mpya na kuwauliza, “kwa nini hamwezi kusikizana na kufikia suluhu katika mzozo huu ambao kwa maoni yangu utachukua miaka mingi kuamuliwa?”

Ndugu hao- Kuldip na Ashman wamepinga uamuzi wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kuwashtaki kwa kughushi stakabadhi ya umiliki wa mali ya Yogesh.

 

Wafikirie tena

Bw Andayi aliwashauri  watatu hao wafikirie tena na tena kuhusu kufikia suluhu ya mzozo huo wa umiliki wa mali.

Kuldip na Ashman wanasisitiza kwamba “hawajagushi hati yoyote kuhusu mali ya ndugu yao mbali ni Dkt Sapra aliyetia sahihi cheti akisema hataki kuwa msimamizi wa mali ya mumewe (ndugu yao) kwa vile anakabiliwa na kesi ya kumuua mumewe.”

Kabla ya kusoma uamuzi uamuzi Bw Andayi aliuliza , “J,  mlalamishi katika kesi hii yuko kortini?”

Dkt Sapra alisimama na kusema, “ Ndiyo mheshimiwa, niko mahakamani.”

“Kuja mbele,” Bw Andayi alimwamuru.

Alipoenda mbele na kusimama kizimbani, hakimu aliwauliza watatu hao , “Je, kuna uwezekano wa kufikia suluhu nje ya mahakama ya  mzozo huu ambao umesikizwa na mahakama karibu zote isipokuwa Mahakama ya Juu?”

 

Siku 40

Alisema amesoma faili zote za kesi hiyo akiandaa uamuzi wake na ameona wakati mmoja wakili Harun Ndubi na Kwame Nkuruma wanaowatetea Kuldip na Ashman pamoja na wakili wa Dkt Sapra walikuwa wameitisha siku 40 watafute suluhu ya mzozo huo wa umiliki wa mali ya Yogesh.

“Je, nyote mnaelewa Kiingereza?” Bw Andayi aliwauliza Kuldip, Ashman na Dkt Sapra.

“Ndio tunaelewa,” walijibu.

Bw Andayi aliwataka mawakili wafanye kikao cha pamoja na kutafuta suluhu ya mzozo huo.

“Kesi hizi za mizozo ya umiliki wa mali huzua uhasama mkali katika jamii. Naamini katika Jamii ya Wahindi kuna Wazee wanaoweza kusuluhisha mzozo huu ikitiliwa maanani Yogesh alifariki na hata kesi hii ikifanywa miaka na mikaka hatafufuka. Hata watoto wake huenda wakachukua mwelekeo mwingine na kuwakatalia mbali wajomba wao na hata kumchukia mama yake (Nisha Sapra),” alisema Bw Andayi.

Marehemu alikuwa amejaliwa watoto watatu  Rishi Sapra (mvulana) , Rakhee na Priya ( wasichana) wanaosoma nchini Canada.

Katika barua waliyoandikia Mahakama Kuu ya Kenya mnamo Juni 22, 2015, wana hao waliambia korti kwamba wangependa wajomba wao Kuldip na Ashman kusimamia mali ya baba yao na wala sio mama yao Dkt Sapra.

Jaji Aggrey Muchelule anayesikiza kesi hiyo ya umiliki wa mali ya Yogesh aliwateua Kuldip na Ashman kusimamia mali aliyoacha mwenda zake.

Kesi itatajwa Machi 13, 2018.