Michezo

Mnunuzi wa Messi sharti aweke mezani Sh89 bilioni – La Liga

August 30th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

VINARA wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wamevuruga mipango ya Manchester City, Paris Saint-Germain (PSG) na Juventus kuhusu uwezekano wa kumsajili nyota Lionel Messi wa Barcelona muhula huu.

Hii ni baada ya La Liga kusema kwamba kifungu na kipengele kinachohitaji kikosi chochote kuweka mezani kima cha Sh89 bilioni ili kumtwaa Messi bado kinafanya kazi na lazima kizingatiwe katika juhudi za kurasimisha uhamisho wa Mwargentina huyo.

Messi, 33, aliwaarifu Barcelona kuhusu azma yake ya kuondoka ugani Camp Nou mnamo Agosti 25 na akasusia shuguli ya kufanyiwa vipimo vya afya mnamo Agosti 30, 2020 kikosi hicho kinapojizatiti kurejea kambini mwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21.

Messi alipania kutumia kifungu kwenye mkataba wake kinachomruhusu kuagana na Barcelona bila ada yoyote. Hata hivyo, Barcelona wanashikilia kwamba makataa ya kuwasilishwa ombi la Messi (Juni 10, 2020) yalipitwa na wakati.

“Tumetathmini mkataba wa sasa wa Messi na Barcelona. Tumebaini kwamba kifungu kinachomfunga ugani Camp Nou bado kinafanya kazi na anayepania kumnunua atalazimika kuweka mezani Sh89 bilioni ili kushawishi Barcelona kumwachilia,” ikasema sehemu ya taarifa ya La Liga kwa kusisitiza kwamba watamwondoa Messi kwenye sajili yao iwapo masharti hayo yatatimizwa.

“Kwa heshima ya mkataba huo, La Liga haitaidhinisha uhamisho wa Messi wala kuondoa jina lake kwenye sajili ya Shirikisho la Soka la Uhispania iwapo mnunuzi hataweka mezani fedha zinazostahili kutolewa ili Barcelona wamwachilie rasmi kuagana nao,” ikaendelea taarifa hiyo.