Makala

Mnyama rahisi kufuga nyumbani, ni mwanamume

Na BENSON MATHEKA August 5th, 2024 2 min read

AKINA dada huwa wanachoma uhusiano wao wa kimapenzi au kuvunja ndoa zao kwa kutojua sanaa ya kuzungumza na wachumba wao. 

Girl child analia uhusiano wake wa kimapenzi aliothamini na kuwekeza hisia na muda ukikatika kwa sababu ya maneno anayoachilia bila kupima athari zake.

Kwa sababu ya mawasiliano chwara ndoa inasambaratika au inabaki gae tu.

Basi leo nakuchanua dada, ujenge mawasiliano thabiti na mtu wako.

Epuka kuzungumza naye kwa ukali. Usimfanye ahisi unashindana naye.

Usijaribu kuhalalisha ukali wako kwa kusema ulikuwa na hasira. Ukiambia mwanamume hivi, utaharibu zaidi.

Dada, mpe mtu wako muda wa kuzungumza. Usitawale mazungumzo, atachukulia unamdharau.

Kuwa thabiti lakini usiwe mwanamke wa kujigamba na kutusi mtu wako.

Matusi yako yataghairi mema yote uliyozungumza naye huko nyuma.

Hakuna mwanamume anayeweza kuvumilia mwanamke anayemtusi.

Thibiti sauti yako. Unaweza kuwa unasema jambo nzuri lakini sauti iharibu uzuri wake.

Wakati mwingine ujumbe wako bomba unakosa kutimiza malengo yake kwa kuwa unauwasilisha vibaya.

Usiwe mtu wa kununa na kumnyamazia mtu wako. Kufanya hivi kunamsukuma mbali.

Kwa ufupi, unamsukuma atoke katika maisha yako. Unaweza kuwa na mtu ndani ya nyumba na awe mbali nawe kwa moyo wake.

Mzungumzie mtu wako kwa lugha tamu kila wakati.

Mjibu, mshirikishe katika mjadala wa masuala ya ustawi na maisha hasa anayopenda na jinsi unavyopenda akutendee.

Ukifanya hivi dada, utaweza mwanamume awe akikuimba. Unapofanya hivi, kumbuka kumtambua kama kichwa cha boma.

Kamwe usitoe kauli anayoweza kusawiri kama ya kumwamrisha au kama wewe ni bosi wake.

Kila wakati ukiwa na mtu wako, dumisha uchangamfu katika mazungumzo yako.

Atanata kwa mazungumzo na atakuheshimu.

Naam, wanaume wanaheshimu wanawake wanaowaondolea stress za maisha na sio kuziongeza. Pamba mazungumzo yenu kwa ucheshi.

Zungumza naye mambo yanayochangamsha akili yake, yanayomfanya ajifunze; inamfanya afurahie kuzungumza nawe. Mazungumzo ya mambo halisi ya watu wazima, sio ya kuigiza.

Kamwe usifanye mazungumzo kati yako na mtu wako yawe ya kumsifu mtu mwingine na kufanya ahisi unamshusha hadhi.

Usimtaje ex wako, usimsifu mchungaji wako, mtu mashuhuri au rafiki yako. Ukifanya hivi utachoma.

Unachosema kionyeshe kwa vitendo, chukua hatua umdhihirishie mtu wako kwamba nafasi yako katika maisha yake sio bahati mbaya; kwamba wewe sio chombo tu cha kuonekana katika maisha yake bali wewe ni sehemu ya maisha yake.

Unaweza kuzungumza kwa vitendo iwapo wewe sio mzuri kwa kusuka mistari.

Kuna waliofanya hivi na wakafaulu, kufeli kwako basi, itakuwa ni kupenda tu. Ikiwa kuna mnyama (ashakum si matusi) rahisi kufuga nyumbani, basi ni mwanamume.