Habari Mseto

Modern Coast yazima safari za Uganda, Rwanda na Tanzania hata kabla ya Kenya kufunga mipaka

March 20th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMPUNI ya uchukuzi wa abiria ya Modern Coast, imesimamisha safari zake zote kutoka Kenya kwenda mataifa ya Tanzania, Uganda na Rwanda, kwa muda usiojulikana, kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kampuni hiyo imetangaza hatua hiyo licha ya kusubiri kwanza serikali ya Kenya itangaze rasmi kwamba imefunga mipaka yake.

Kufikia sasa kile serikali imefanya ni kuamuru wageni wote wachunguzwe mipakani.

Kwenye taarifa iliyotolewa Alhamisi, Modern Coast ilisema kuwa hatua hiyo pia itaathiri huduma za mabasi kutoka mataifa hayo matatu kuja Kenya kuanzia Machi 19, 2020.

“Huduma katika ruti zilizotajwa hapo zitasimamishwa kwa muda usiojulikana. Hata hivyo, tutakuwa tukifuatilia ushauri kutoka kwa Serikali na Wizara ya Afya kuhusiana na janga la virusi vya corona,” ikasema taarifa hiyo.

Abiria wote walioathiriwa na hatua hiyo wametakiwa kuwa kuwasiliana na Afisi Kuu ya kampuni hiyo kupitia simu nambari +254709897000 au wafike katika matawi yoyote ya kampuni ili warejeshewe nauli walizokuwa wamelipa.