Mohamed Salah asema atasalia Liverpool msimu ujao

Mohamed Salah asema atasalia Liverpool msimu ujao

Na MASHIRIKA

FOWADI matata wa Liverpool, Mohamed Salah, 29, amesema ana uhakika wa asilimia 100 kuwa atasalia kambini mwa kikosi hicho msimu ujao na ana imani kuwa kauli yake hiyo itakomesha kabisa mijadala yoyote kuhusu iwapo atatia saini mkataba mpya ugani Anfield au la.

Kandarasi ya sasa kati ya Salah na Liverpool inatarajiwa kukatika rasmi mnamo Juni 2023, jambo linalozua tetesi kuhusu uwezekano wa kuuzwa kwake au iwapo Liverpool watakuwa radhi kumwachilia ayoyomee anakopenda chini ya kipindi cha mwaka mmoja ujao.

“Nisingependa kuzungumzia kuhusu mustakabali wangu kitaaluma zaidi ya hapo. Muhimu zaidi kwa sasa kwangu ni kuona Liverpool wakitwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA),” akasema Salah atakayekuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Liverpool dhidi ya Real Madrid ya Uhispania mnamo Mei 28, 2022 jijini Paris, Ufaransa.

Sadio Mane ambaye pia ni mshambuliaji wa Liverpool amesema atatangaza maamuzi yake ya ama kusalia Liverpool au kuondoka ugani Anfield mwishoni mwa msimu huu baada ya kukamilika kwa fainali ya UEFA kati yao na Real.

Kufikia sasa, nyota huyo raia wa Senegal amefungia Liverpool mabao 120 kutokana na mechi 268 na ataingia katika miezi yake 12 ya mwisho kambini mwa Liverpool mnamo Juni 2022.

Salah alijiunga na Liverpool mnamo 2017 baada ya kuagana na AS Roma ya Italia. Amefungia Liverpool mabao 156 kutokana na mechi 253. Alisaidia pia Liverpool kutwaa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2019-20, taji la UEFA mnamo 2019, Kombe la Dunia 2020, Uefa Super Cup mnamo 2020 na Kombe la FA pamoja na Carabao Cup 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Utengano kati ya Uhuru na Ruto wadhihirika hata katika...

Montreal yapiga hatua ya kuingia Klabu Bingwa CONCACAF kwa...

T L