Habari

Moi afanyiwa uchunguzi wa kiafya jijini Nairobi

October 14th, 2019 1 min read

Na ERIC MATARA

RAIS Mstaafu Daniel Arap Moi mnamo Jumapili alipelekwa katika The Nairobi Hospital katika kile familia na watu wa karibu naye wamesema ni ukaguzi wa kimatibabu wa kawaida.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano muhimu ya Mzee Moi, Bw Lee Njiru ameambia Taifa Leo alipelekwa hospitalini ambapo pia daktari wake binafsi David Silverstein alikuwepo.

“Ndio, ninathibitisha kwamba Mzee Moi amefika The Nairobi Hospital kukaguliwa hali yake ya afya. Ni muhimu kwa mwanadamu yeyote kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu; hivyo hakuna jambo la kuibua taharuki,” alisema Bw Njiru.

Hata hivyo, hakufichua ni uchunguzi wa aina ipi ambao Rais huyo wa zamani alifanyiwa.

Oktoba 10 ilikuwa sikukuu ya Moi Dei ambapo Mzee mwenyewe alikuwa nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru ambapo alitangamana na familia na marafiki.