Habari MsetoSiasa

Moi afuata nyayo za Ruto kujijenga kisiasa Bondeni

May 22nd, 2019 2 min read

BARNABAS BII Na WYCLIFF KIPSANG

MWENYEKITI wa Chama cha Kanu, Bw Gideon Moi, amekuwa akikutana na wazee wa jamii na watu wenye ushawishi katika mikakati yake mpya ya kujiimarisha kisiasa na kuvutia wapigakura akilenga uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Moi ambaye ni Seneta wa Baringo na hasimu mkubwa wa Naibu Rais William Ruto katika eneo la Rift Valley, amekuwa akifanya ziara za kukutana na watu ili kupigia debe chama cha Kanu kwa kukutana na jumbe za wazee, wafanyabiashara, viongozi wa kisiasa na washikadau wengine mashinani. Amekuwa pia akiandaa mikutano ya hadhara.

Katika mikakati yake ya hivi punde ya kujenga uhusiano na wapigakura, Seneta Moi alikutana na wazee na viongozi kutoka maeneo ya Rift Valley na Magharibi katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki huko Sugoi, ngome na nyumbani kwa Dkt Ruto.

Naibu Rais amekuwa akifanya mikutano aina hiyo nyumbani kwake Karen jijini Nairobi na vilevile Sugoi katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Kabla ya kukutana na jumbe hizo, Seneta Moi alikutana faraghani na kikundi cha wakulima kujadili masuala yanayotatiza sekta ya Kilimo katika juhudi za kujijenga kisiasa eneo lenye wapigakura wengi la Rift Valley.

Chama cha Jubilee ambacho Bw Ruto anatoka, kina ufuasi mkubwa Rift Valley japo Kanu na Chama cha Mashinani cha aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto vimepenya eneo hilo na kunyakua washirika muhimu wa Naibu Rais

“Tumejitolea kujenga mtandao wa kisiasa wenye nguvu kwa sababu umeonyesha una uwezo wa kuunganisha Wakenya,” alisema Bw Ernest Kirui, mmoja wa wazee wa Baraza la Wazee la jamii ya Wakalenjin maarufu kama Myoot ambao walihudhuria mkutano katika nyumba ya mwafanyabiashara Sammy Kogo eneo la Sugoi.

Hata hivyo, wazee hao walimweleza Seneta Moi kwamba anafaa kutangaza wazi azima yake ya kugombea urais.

Japo hajatangaza hadharani azima yake ya kugombea urais, Seneta Moi amekuwa akivamia ngome ya Naibu Rais akitaka mabadiliko katika sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa eneo hilo.

Majuzi, alifanya mkutano wa faragha na viongozi na wakulima katika hoteli moja mjini Eldoret ambako alipendekeza mabadiliko kadhaa katika sekta hiyo. Hii ilikuwa mara ya pili mwenyekiti huyo wa Kanu kufanya mkutano kama huo na wandani wa Naibu Rais wanachukulia hatua hiyo kama mikakati ya kumzima kisiasa eneo hilo.