Habari MsetoSiasa

Moi alivyoenzi Nakuru, eneo la makazi yake ya kifahari ya Kabarak

February 5th, 2020 2 min read

NA ERICK MATARA

KATIKA kipindi cha utawala wake wa miaka 24, Rais Mstaafu Daniel Moi alipenda sana mji wa Nakuru ambako pia ana makazi ya kifahari ya Kabarak katika eneobunge la Rongai.

Mzee Moi kila mara alifika Nakuru nyakati za wikendi au mkesha wa mwaka mpya ili kuhepa hekaheka za kisiasa zilizotawala mji wa Nairobi na kuja kutulia kwenye mandhari ya kuridhisha ya Nakuru.

Baadhi ya wakazi wa Nakuru walieleza jinsi alikuwa akiwaalika watu mbalimbali katika mji wa Ikulu ya Nakuru na hata kuongoza mikutano ya serikali humo.

“Tulikuwa na uhakika kila wikendi kwamba Mzee Moi angefika Nakuru kutokana na mapenzi yake kwa mji wetu. Hali ilikuwa hivyo hivyo kila mkesha wa mwaka mpya na kwa kweli alikuja,” akasema mkazi kwa jina Gilbert Kabage.

“Kabla kubadilishwa kuwa ikulu, jengo hilo lilikuwa afisi za mkuu wa mkoa. Baada ya kutwaa mamlaka kutoka kwa hayati Mzee Jomo Kenyatta mnamo 1978, Rais Moi alikuwa akitembelea Nakuru kujiburidisha na kuandaa mikutano na marafiki na pia mawaziri,” akasema mkazi mwengine Jesse Karanja.

Mapenzi ya dhati kwa mji wa Nakuru yalianza kukolea kwa Mzee Moi wakati alikuwa makamu wa Rais ambako alinunua ardhi kubwa eneo la Kabarak alikojenga makazi yake ya hadhi.

Kwenye kitabu chake, Beyond Expectations, From Charcoal to Gold, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi marehemu Njenga Karume aliandika kwa kina jinsi Mzee Moi alivyonunua ardhi hiyo ya Nakuru.

Kitabu hicho kinaeleza aliinunua kupitia mashauriano na Mzee Jomo Kenyatta baada ya kuondoka kwa wakoloni waliokuwa wametwaa vipande vikubwa vya ardhi maeneo mbalimbali nchini.

“Mzee Kenyatta alimweleza Moi kwamba alikuwa anamiliki vipande vingi vya ardhi ilhali makamu wake hakuwa na chochote. Hii ndiyo ilimchochea Moi kununua ardhi Kabarak na vipande vingine vya ardhi maeneo tofauti nchini,” akaandika marehemu Bw Karume katika kitabu hicho.

Baada ya kujenga makazi yake Kabarak, alikuwa akitumia ikulu kuandaa mikutano mingine huku mara nyingi akipumzika na kujistarehe kwake.

Hata hivyo, alihakikisha maafisa kutoka kitengo cha GSU walikuwa wakitoa ulinzi ikuluni huku wafanyakazi karibu 50 wakitunza jengo hilo kuhakikisha lipo imara na linaafiki hadhi ya kutumiwa na Rais.

Kama tu wanasiasa wengine nchini wanaopenda kuishi maisha ya kifahari, makazi ya Mzee Moi Kabarak ni ya thamani ya mamilioni ya fedha na yanaweza kulinganishwa tu ikulu.

Ingawa hivyo, ana makazi mengine saba, sita katika eneo la Bonde la Ufa na moja jijini Nairobi ambayo pia alipenda kuishi akiwa na shughuli jijini baada ya kustaafu.

Mbunge wa Rongai ni Raymond Moi ambaye anahudumu muhula wake wa pili na ni mwanawe Rais huyo mstaafu. Alichaguliwa kupitia chama cha KANU alichotumia Mzee Moi kuingia ikuluni kipindi chote cha utawala wake.

Pia anamiliki mashamba makubwa katika maeneo ya Subikia, Naivasha, Gilgil, Bahati, Molo, Njoro na Rongai japo aliamua kuishi Kabarak baada ya kustaafu siasa.

Gavana wa Nakuru Lee Kinyajui anasema kwamba uwekezaji na miradi aliyoianzisha Mzee Moi Nakuru, imesaidia sana kuinua kaunti hiyo kiuchumi.